Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa kuamini Hodhi na kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana hodhi ambayo Ummah wake siku ya Qiyaamah wataijia. Upana wake ni kama urefu wake na ni sawa na masafa ya safari ya mwezi. Vikombe vyake ni sawa na idadi ya nyota mbinguni, kama yalivyopokelewa mapokezi Swahiyh kupitia njia nyingi.

MAELEZO

Miongoni mwa mambo ambayo ni lazima kuyaamini ni Hodhi tukufu siku ya Qiyaamah. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini juu ya uwepo wake kwa mujibu wa Hadiyth Swahiyh na za wazi juu ya jambo hilo. Mu´tazilah na Khawaarij wameikanusha kwa sababu ya ujinga wao na kupondoka kwako kutokamana na Qur-aan na Sunnah. Kwa hivyo hawastahiki kunywa kutoka ndani yake. Wao ni katika wapotofu wabaya zaidi na Ahl-ul-Bid´ah wenye kupotosha.

Hapana shaka kwamba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amempa Mtume Wake Kawthar na akampa Hodhi. Kawthar ni katika aina ya Hodhi; inamwaga ndani ya Hodhi.

Hodhi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Qiyaamah ni kwa ajili ya wafuasi wake, Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambao hawakubadili wala hawakugeuza. Wataiendea wakiwa wenye kiu. Yule mwenye kunywa ndani yake mara moja basi kamwe hatohisi kiu. Sote tunamuomba Allaah, Malaika Wake watukufu na wanachuoni wanashuhudia ya kwamba tunaamini Hodhi na Kawthar. Tunatarajia kunywa ndani yake kama ilivyosifiwa na Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa urefu wake ni kama upana wake, ni sawa na masafa ya safari, maji yake ni meupe zaidi kushinda maziwa, matamu zaidi kuliko asali. Yule atakayekunywa mara moja tu basi kamwe hatohisi kiu. Vikombe vyake ni sawa na idadi ya nyota mbinguni. Ummah wataiendea Hodhi wamkute Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa karibu na Hodhi na afurahishwe na Maswahabah zake. Kundi la watu watataka kuiendea Hodhi wazuiwe na Malaika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nitawasubiri kwenye Hodhi. Tahamaki ajitokeze mtu ambaye atawafukuza mbali na Hodhi yangu siku ya Qiyaamah kama anavyofukuzwa ngamia aliyepotea. Nitawaita, lakini kusemwe: “Walibadilisha baada yako”, ambapo nitasema: “Tokomeeni! Tokomeeni!”[1]

Watafukuzwa mbali na Hodhi kwa sababu ya upotevu na upotashaji wao duniani.

[1] Muslim (249).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 15/10/2019