29. Adabu za kuzingatia wakati mwanamke anatoka kwenda msikitini

6 – Akitoka kwenda msikitini basi ni lazima kuchunga adabu zifuatazo:

1 – Awe ni mwenye kujisitiri kwa mavazi na Hijaab kamilifu. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Wanawake walikuwa wakiswali pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kisha wanaondoka zao hali ya kujigubika mavazi yao. Hakuna yeyote awezae kuwajua kwa sababu ya giza.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

2 – Watoke pasi na kujitia manukato. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiwazuie wajakazi wa Allaah kutokamana na misikiti ya Allaah na watoke bila ya kujitia manukato.”

Ameipokea Ahmad na Abu Daawuud.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke yeyote aliyejifukiza udi basi asihudhurie pamoj na sisi ´Ishaa ya mwisho.”

Ameipokea Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaa´iy.

Muslim amepokea kutoka kwa Zaynab, ambaye ni mke wa Ibn Mas´uud:

“Atapohudhuria mmoja wenu msikiti basi asijifukize udi.”

Imaam ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Ndani yake kuna dalili inayoonyesha kuwa kutoka kwa wanawake kwenda misikitini inafaa tu pale ambapo jambo hilo halitoandamana na fitina na yale yenye kuamsha fitina kama mfano wa udi.” Akasema: “Kimechopata kufahamika kupitia Hadiyth ni kwamba wanaume kuwapa idhini wanawake kwenda misikitini ni pale ambapo hakuna yale yanayoita katika fitina kama vile manukato, mapambo kama ya dhahabu au pambo lolote.”[1]

3 – Asitoke akiwa amejipamba kwa mavazi na mapambo mengine. Mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Lau Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwaona wanawake yale tunayoyaona basi angeliwazuia kutokamana na msikiti kama ambavo wana wa Israaiyl waliwazuia wanawake zao.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Imaam ash-Shawkaaniy amesema katika “Nayl-ul-Awtwaar”:

“Maneno ya ´Aaishah “Lau angeliona yale tunayoyaona” anamaanisha urembo wa mavazi yao, manukato, mapambo na kuonyesha mapambo. Wanawake walikuwa wakitoka katika zile nguo nzito na zenye kuenea.”[2]

Imaam Ibn-ul-Jawziy (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu “Ahkaam-un-Nisaa´”:

“Mwanamke anatakiwa kutahadhari kutokamana na kutoka kwa kiasi atavyoweza. Akisalimika juu ya nafsi yake basi watu hawatosalimika naye. Akilazimika kutoka basi atoke kwa idhini ya mume wake katika sifa na pambo baya na afanye njia yake ni katika mahali palipoepukana na watu na si mabarabarani na masokoni, pia ajilinde kusikiliwa sauti yake, atembee kandokando ya njia na si katikati yake.”[3]

[1] (03/140-141).

[2] (03/140-141).

[3] Uk. 39.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 58-60
  • Imechapishwa: 04/11/2019