28. Watoto wa Kiislamu wanatakiwa kudhibitiwa

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Imepokelewa kwamba wanatakiwa kuamrishwa kuswali wanapokuwa na miaka saba na wapigwe kwayo wanapofikisha miaka kumi na pia watenganishwe katika malazi.

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapokuwa na miaka saba  na wapigeni kwayo wanapofikisha miaka kumi na pia watenganisheni katika malazi.”[1]

Mtoto wa miaka saba anatakiwa kuamrishwa swalah anapokuwa na miaka saba. Mtoto wa miaka saba anakuwa na uwezo wa kupambanua na anatambua.

Wanatakiwa wapigwe kwayo wakizembea kwayo ilihali wameshakuwa na miaka kumi. Kwa sababu kipindi hicho ima wamekaribia kubaleghe au tayari wamekwishabaleghe. Ama mtoto mdogo akiacha kuswali hatakiwi kupigwa kwa sababu haijamlazimu. Hata hivyo anatakiwa kupewa malezi ya swalah. Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“… pia watenganisheni katika malazi.”

Msiwaache wamoja wakalala kando ya wengine. Kuna khatari shaytwaan akawapambia machafu na hivyo wakafitinishwa. Haya yanawahusu watoto wa kiume na watoto wa kike. Hata wavulana wasiachwe wakalala pambizoni na wavulana wengine, wasichana wasiachwe wakalala pambizoni na wasichana wengine na wavulana wasiachwe wakalala pambizoni na wasichana. Wanatakiwa kutenganishwa katika malazi kwa ajili ya kuchelea fitina. Watoto wanatakiwa kudhibitiwa na wasipuuzwe.

Hapa tuna mambo matatu muhimu:

1 – Watoto wanatakiwa kuamrishwa kuswali ili waizowee. Swalah hiyo inasihi na inakuwa ni ya sunnah. Wasipigwe ikiwa hawakuswali kwa sababu hawakuacha jambo la lazima kwao. Katika swalah kunaingia vilevile kutawadhisha. Wanatakiwa kuamrishwa kutawadha na kuwafunza namna ya kutawadha.

2 – Wanapofikisha miaka kumi na wasiswali basi wapigwe kwayo. Kwa sababu katika kipindi hicho ima wawe wamekwishabaleghe au wamekaribia kubaleghe. Wanatakiwa kuadhibiwa wakiacha jambo la lazima.

3 – Wanapofikisha miaka kumi kuna khatari juu yao ya matamanio. Kwa hivyo watenganishwe katika malazi. Hii ni moja ya zile dalili zinazokataza wanawake kuchanganyikana na wanamme.

[1] Abu Daawuud (495). Hadiyth ni Swahiyh. Tazama ”Naswb-ur-Raayah” (1/298) kwa tamko kama hilo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 27
  • Imechapishwa: 14/07/2021