28. Wakanushaji na wafananishaji wamekusanya kati ya ukanushaji na ufananishaji


Mkanushaji ni yule anayekanusha kitu katika majina au sifa za Allaah. Kama mfano wa Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah.

Mfananishaji ni yule anayemthibitishia Allaah sifa hali ya kuzifananisha na za viumbe Wake. Kama mfano wa wahenga wa Raafidhwah.

Uhakika wa mambo ni kwamba kila mkanushaji ni mfananishaji na kila mfananishaji ni mkanushaji. Kuhusu mkanushaji ukanushaji wake uko wazi. Kufananisha kwake sifa za Allaah na sifa za viumbe kunakuja namna ya kwamba ameamini kuwa kuthibitisha sifa za Allaah kunapelekea kushabihisha. Matokeo yake hilo likamfanya kukanusha sifa za Allaah akiwa ni mwenye kukimbia hilo. Hivyo akawa ni mwenye kufananisha kwanza kisha ndio akakanusha. Kuhusiana na mfananisha kufananisha kwake kuko wazi. Ama kukanusha kwake kunapatikana kwa njia tatu zifuatazo:

Ya kwanza: Amekanusha andiko linalothibitisha sifa kwa vile ameligeuza kinyume na udhahiri wake. Hakika andiko linatoa dalili kuthibitisha sifa yenye kulingana na Allaah. Andiko halitoi dalili juu ya kufanana sifa za Allaah na za viumbe Wake.

Ya pili: Akimfananisha Allaah na viumbe Wake basi amekanusha maandiko yote ni yenye kutoa dalili juu ya kwamba Allaah hafanani na viumbe Wake. Kwa mfano amesema (Ta´ala):

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua mwenye jina kama Lake?”[1]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.”[2]

Ya tatu: Akimfananisha Allaah na viumbe Wake basi amemkanushia ukamilifu Wake ambao ni wa wajibu. Hilo linapatikana kwa njia ya kwamba amemshabihisha Mola mkamilifu na viumbe wapungufu kwa njia zote.

[1] 19:65

[2] 112:04