Aayah za sehemu ya mwisho zote zinazungumzia upamoja ambao ni wa kimaalum (al-Ma´iyyah al-Khaasswah) na upamoja ulioenea (al-Ma´iyyah al-´Aammah). Amesema (Ta´ala):

a) Allaah yuko pamoja na waja Wake wote kwa ujuzi Wake

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

”Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anajua yanayoingia ardhini, na yatokayo humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo, Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuyaona.” (57:04)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) anakijua kila kitu kilicho mbinguni na ardhini, kilichopita na kitakachokuja. Yote hayo anayajua. Pamoja na hivyo Yeye anakuwa pamoja na waja Wake popote wanapokuwa. Bi maana anakuwa pamoja nao kwa ujuzi Wake na wakati huo huo yuko juu ya ´Arshi. Anakuwa pamoja nao kwa elimu Yake yenye kuwazunguka isiyofichikana na kitu. Amesema (Ta´ala):


لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

“… ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi Wake.” (65:12)

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.” (08:75)

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Hauwi mnong’ono wa [watu] watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala [hauwi mnong’ono wa] chini kuliko ya hivyo, na wala wa wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao popote watakapokuwa; kisha Atawajulisha kwa yale [yote] waliyoyatenda Siku ya Qiyaamah – hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.” (58:07)

Amemalizia Aayah hii kwa ujuzi kwa lengo ili msomaji na msikilizaji ajue kuwa kinachokusudiwa ni elimu na wakati huo huo yuko juu ya ´Arshi (Jalla wa ´Alaa) na kwamba hafichikani na kitu (Jalla wa ´Alaa).

b) Allaah yuko pamoja na waja Wake wema kiujuzi, kwa kuwanusuru na kwa kuwapa nguvu

Hali kadhalika inahusiana na upamoja wa kimaalum:

لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

“Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi.” (09:40)

Haya yalisemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) wakati walipokuwa pangoni.

إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ

”Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona.”(20:46)

Wanaambiwa Muusa na Haaruun (´alayhimaas-Salaam).

وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

”Subirini. Hakika Allaah Yu Pamoja na wanaosubiri.”(08:46)

كَم مِّن فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Makundi mangapi machache yameshinda makundi mengi kwa idhini ya Allaah? Na Allaah Yu pamoja na wenye kusubiri.”(02:249)

Aayah zote hizi ni zenye kufahamisha upamoja ambao ni maalum ambapo anakuwa pamoja na mawalii Wake, wenye kumtii na Mitume Wake kwa kuwazunguka kielimu, kinusura na kuwapa nguvu.

Ama kuhusu upamoja wa kijumla unahusiana na kukizunguka kila kitu kielimu na kwamba hafichikani na chenye kufichikana na kwamba Yeye ndiye mwenye kuwaendesha na kuwapeleka.

Upamoja wa kimaalum unakuwa na Ujuzi pamoja vilevile na kuwanusuru mawalii Wake na kuwahami. Kama Alivyosema kupitia ndimi ya Mtume Wake alipomwambia Swahabah wake pindi walipokuwa pangoni:

لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

“Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi.” (09:40)

Akamwambia Muusa na Haaruun (´alayhimaas-Salaam) walipokuwa mbele ya Fir´awn. Allaah aliwahami kutokana na shari yake:

إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ

”Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona.” (20:46)

Hali kadhalika viumbe wote Yuko pamoja nao kwa ujuzi Wake inayokijua kila kitu. Anazijua siri zao na yale wanayonong´onezana na wakati huo huo yuko juu ya ´Arshi. Elimu Yake imekizunguka kila kitu. Anajua na kuona mdudu mchungu mweusi katika usiku wenye giza kingi. Anajua jinsi yanavyoenda maji ya mito na bahari na vilivyo ndani yavyo. Anajua vyote vilivyomo chini ya ardhi na vinavyohadithiwa na mioyo. Vyote hivyo hakuna kinachofichikana Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ

“Na hushughuliki katika jambo lolote na wala husomi humo chochote katika Qur-aan, na wala hamtendi ‘amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo.” (10:61)

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئِينَ وَالنَّصَارَىٰ وَالْمَجُوسَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا إِنَّ اللَّـهَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ

“Hakika wale walioamini, na ambao Mayahudi, na Wasabai [waabudiao nyota], na Manaswara, wa Majusi [waabudiao moto], na wale wanaoshirikisha; hakika Allaah Atahukumu baina yao Siku ya Qiyaamah. Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Mwenye kushuhudia.” (22:17)

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

“… ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi Wake.” (65:12)

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Mjuzi.” (08:75)

وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ

“Na mwanamke yeyote yule habebi [mimba] na wala hazai isipokuwa kwa ujuzi Wake.” (35:11)

Elimu Yake imewazunguka viumbe. Ujuzi Wake maalum uko pamoja na mawalii Wake. Anazijua hali za viumbe Wake maalum na wengineo. Anayajua yatayokuja katika zama za mwisho. Anayajua yatayokuja siku ya Qiyaamah. Anayajua yaliyopita katika zama za kale. Yote hayo anayajua. Bali anayajua na ameyazunguka (Jalla wa ´Alaa).

Ni wajibu kumthibitishia nayo (Subhaanahu wa Ta´ala) na sambamba na hilo kumtakasa kushabihiana na viumbe Vyake kwenye kitu katika sifa Zake (Jalla wa ´Alaa). Haya ndio maoni ya watu wa haki ambao ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com