28. Unasemaje juu ya kwamba vitabu vya ´Aqiydah havitatui matatizo ya wakati wa sasa?

Swali 28: Nimesoma kitabu kinachoitwa “Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah” cha Muhammad Suruur bin Nayif Zayn-ul-´Aabidiyn ambapo amesema:

“Nimesoma vitabu vya ´Aqiydah na kuona kuwa havikuandikwa katika wakati wetu. Vilikuwa ni vyenye kutatua migogoro ya wakati ule vilipoandikwa. Leo kuna migogoro ambayo inahitaji ufumbuzi mpya. Kwa sababu usulubu katika vile vitabu vya kale si wenye kuridhisha. Kwa sababu vina maandiko na hukumu. Kwa ajili hiyo ndio maana vijana wengi wamevipa mgongo na kuvisusa.”[1]

Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Wako ambao wanataka kuwakimbiza watu mbali kusoma ´Aqiydah na vitabu vya Salaf. Wanakimbiza watu na vitabu vya maimamu wa Uislamu. Wanachotaka ni kuwafanya vijana wasome vitabu vyao, vitabu vya wao na wajinga mfano wao na vitabu vya watu wa propaganga wapotevu. Mtu huyu ni katika watu wa propaganda wapotevu. Ni wajibu kwetu kutahadhari kitabu chake na kutahadharisha naye.

Ninakuelezeni kuwa Shaykh Muhammad Amaan al-Jaamiy amerikodi kanda nzima kuhusu sentesi hii:

“Kwa sababu usulubu katika vile vitabu vya kale si wenye kuridhisha. Kwa sababu vina maandiko na hukumu.”

Ameiraddi Radd safi kabisa. Itafuteni kanda hiyo na muisambaza kati ya waislamu ili waweze kujiepusha na mtu huyu mbaya na watahadhari kutokana na shari hii yenye kuingia ndani ya miji ya waislamu. Kanda hii ni nzuri sana. Allaah amjaze kheri Shaykh wetu Muhammad Amaan al-Jaamiy na aunusuru Uislamu na waislamu kupitia kwake[2].

Ni kwa nini tunaleta fikira kutoka nchi za nje? Ni kwa nini tunaleta fikira kama hizi kutoka kwa Muhammad Suruur Zayn-ul-´Aabidiyn London au wengineo kutoka maeneo hayo?

Ni kwanini haturejei katika vitabu vya Salaf na vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni wa Tawhiyd? Ni kwa nini tunarejea katika vitabu vya waandishi au wafikiriaji ambao malengo yao na kiwango chao cha kielimu hakijulikani?

Huyu huyu Muhammad Suruur anawapoteza vijana kwa maneno yake haya na kuwakimbiza mbali na vitabu  vya ´Aqiydah sahihi na vitabu vya Salaf. Anawapotosha kwenda katika fikira mpya na vitabu vipya vilivyobeba fikira zenye kutia mashaka. Kwa mtazamo wa Muhammad Suruur maandiko na hukumu vilivyomo katika vitabu vya ´Aqiydah ndio mambo yenye kuleta matatizo; vitabu vinavyonukuu aliyosema Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anataka fikira za fulani na fulani. Hataki maandiko na hukumu. Tahadharini na njama hizi batili ambazo malengo yake ni kutaka kuwakimbiza mbali vijana wetu na vitabu vya Salaf.

Himdi zote njema anastahiki Allaah kuona Salaf wametuachia vitabu vya kutosheleza vyenye kutatua mambo ya ´Aqiydah na ulinganizi. Tofauti na maneno ya mwandishi huyu ya kwamba si vyenye kuridhisha. Ni vitabu vya kielimu na vina vyanzo katika Qur-aan na Sunnah. Kutokamana na Qur-aan, ambayo haiingiliwi na batili mbele wala nyuma yake, kuna vitabu kama “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy, “as-Swahiyh” ya Muslim na vitabu vingine vya Hadiyth. Halafu kuna vitabu vya Sunnah kama “as-Sunnah” ya Ibn Abiy ´Aaswim, “ash-Shariy´ah” ya al-Aajurriy, “as-Sunnah” ya ´Abdullaah bin Imaam Ahmad, vitabu vya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, vitabu vya mwanafunzi wake Ibn-ul-Qayyim na vitabu vya Shaykh-ul-Islaam na muhuishaji Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab – lazimianeni na vitabu hivi!

Kipofu tu ndiye mwenye kusema kuwa Qur-aan, Sunnah na maneno ya wanazuoni wenye kuzingatiwa haviridhishi. Mshairi amesema:

Kuna uwezekano jicho lisione mwanga kwa sababu ya ugonjwa wa macho [tongotongo]

kuna uwezekano mdomo usihisi ladha ya maji kwa sababu ya ugonjwa

´Aqiydah haichukuliwi isipokuwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah, na sio kutoka katika fikira za watu.

[1] Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah, uk. 08.

Mtu huyu fikira zake zilizopinda zimefichuka kupitia vitabu vyake na uadui wake kwa Ahl-us-Sunnah Saudi Arabia. Tuliyoshuhudia ni yale aliyoandika mwenyewe. Hapa kunafuatia baadhi ya mifano juu ya hilo:

1 – Chuki yake dhidi ya vitabu vya ´Aqiydah, jambo lenye kudhihiri katika swali lililoulizwa hapo juu.

2 – Ana ´Aqiydah ya Khawaarij pale anapowakufurisha watawala na wananchi kwa sababu tu madhambi. Kuhusu watawala, makala zake katika gazeti la “as-Sunnah” limejaa hayo. Ama kuhusu wananchi, anaonelea kuwa watu wa Luutw (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lau wangeliamini na wakaendelea kufanya madhambi yao machafu basi imani yao kumuamini Allaah isingeliwanufaisha chochote. Amesema:

“Sio jambo la kushangaza kuona liwati ndio ilikuwa suala muhimu zaidi katika ulinganizi wa Luutw (´alayhis-Salaam). Lau wangeliitikia na kumuamini Allaah na kuacha shirki, basi isingelikuwa na maana yoyote endapo wasingeacha dhambi na tabia zao mbaya ambazo walikuwa wamekusanyika juu yake.” (Manhaj-ul-Anbiyaa’ fiyd-Da´wah ilaa Allaah, uk. 158)

Anakufurisha kwa dhambi kubwa pasi na kifungamanishi hata kama mtendaji hahalalishi kitendo hicho.

3 – Uadui wake kwa Ahl-us-Sunnah Salafiyyuun. Hapa utajisomea mwenyewe namna ambavyo anawabeza, kuwatukana na kuwaangusha wanazuoni wa Salafiyyah Saudi Arabia na khaswa wanazuoni wa baraza la Kibaar-ul-´Ulamaa´. Amesema chini ya kichwa cha khabari “al-Musaa´daat ar-Rasmiyyah”:

“Aina nyingine ya watu inachukua misaada ya serikali na kufungamanisha nafasi zao na nafasi za mabwana wao… Pindi mabwana wanapochukua msaada kutoka kwa wamarekani ndipo utawaona waja upesi wanakusanya dalili zenye kujuzisha kitendo hicho na kuwakataza wengine wote wenye kuonelea kinyume. Wakati mabwana wanapotofautiana na Iraan utawaona waja upesi wanataja ubaya wa Raafidhwah… Na pale ambapo ugomvi unaisha watumwa wananyamaza na kuacha kueneza vitabu walivyopewa. Kundi hili la watu wanasema uwongo… wanafanya ujasusi…  wanachukua uamuzi… na wanafanya kila kitu ambacho mabwana zao wanawaamrisha. Watu hawa ni wachache na himdi zote njema ni za Allaah. Wamejipenyeza katika ulinganizi na kazi za Kiislamu. Wamefichuka hata kama wana ndevu ndefu na mavazi mafupi na wakadai ya kwamba ni watetezi wa Sunnah. Ulinganizi wa Kiislamu haudhuriki uwepo watu aina hii. Unafiki ni kitu cha tangu kale. Enyi ndugu! Msidanganyike na uinje huu. Kundi hili la watu limeundwa na madhalimu. Kazi ya Shaykh muheshimiwa haitofautiani na kazi ya mkuu wa polisi.” (Gazeti “as-Sunnah”, toleo la 23, Dhul-Hijjah 1412, uk. 29-30))

Ni jambo la wazi kabisa ya kwamba aina nyingine ya watu anawalenga wanazuoni wa Saudi Arabia na mabwana anakusudia watawala wa Saudi Arabia. Kinachotilia nguvu hilo ni maneno yake:

“Pindi mabwana wanapochukua msaada kutoka kwa wamarekani ndipo utawaona waja upesi wanakusanya… “

Anakusudia vita vya Ghuba. Waja anaowazungumzia ni wanazuoni wetu – Allaah amlipe kile anachostahiki. Kisha isitoshe anawatuhumu unafiki.

Amesema tena chini ya kichwa cha khabari “al-Mustabidduun wal-´Abiyd”:

“Utumwa wa leo umejengwa katika tabaka mbalimbali ya piramidi.”

Mosi: Juu ya kiti amekaa raisi wa Marekani George Bush na kesho anaweza kuwa Clinton.

Pili: Viongozi katika miji ya waarabu. Wanaamini kuwa manufaa yao na madhara yao yako mikononi mwa Bush.”

Amelijuaje hilo? Je, amezifungua nyoyo zao? Wamesema hivo?

سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ

“Kutakasika na mapungufu ni Kwako – huu ni usingiziaji wa dhuluma mkubwa mno!” (24:16)

Anaendelea na makala yake na kusema:

“Kwa ajili hii ndio maana wanahiji kwenda kwake na wanamfanyia nadhiri na vitu vya kujikurubisha.”

Hii ni dalili yenye kuonesha kuwa anawakufurisha watawala wote. Anaendelea na makala yake na kusema:

Tatu: Wenye kuwafuata viongozi wa waarabu katika mawaziri, mawakili wa mawaziri, majenerali na washauri.  Hawa wanafanya unafiki kwa viongozi wao na wanawapambia viongozi wao batili yote pasi na kuona hayaa wala heshima.

Nne, tano na sita: Viongozi wa ngazi za juu wakiwa kwa mawaziri.

Hapo kabla utumwa ilikuwa ni jambo jepesi; mtumwa alikuwa na mawasiliano na mmiliki wake moja kwa moja. Lakini hii leo utumwa unachanganya. Siachi kushangazwa na wale wenye kuzungumzia Tawhiyd pamoja na kuwa ni watumwa wa watumwa ambao ni watumwa wa watumwa ambao ni watumwa wa watumwa ambao ni watumwa wa watumwa ambao mabwana wao mtu mmoja ambaye ni mnaswara.”

Ni kina nani wenye kuzungumzia Tawhiyd? Je, si ni wanazuoni wa Saudi Arabia kama Ibn Baaz, Ibn ´Uthaymiyn, Swaalih al-Luhaydaan, Swaalih al-Fawzaan na ndugu zao katika wanazuoni wakubwa? Leo kuna watu wenye kuwatuhumu kuwa ni watumwa wa watawala na kwa njia hiyo vilevile watumwa wa Bush. Amesema kweli Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Ukiwa huna hayaa basi fanya utakalo.” (al-Bukhaariy (3296))

Kisha isitoshe ni mwenye kujigonga. Yeye anaharamisha kuchukua msaada kutoka kwa makafiri wakati wa dharurah wakati yeye mwenyewe anaomba ulinzi kwao na anaishi kwenye nchi yao na chini ya ulinzi wao. Ni ipi tofauti kati ya makafiri wa Marekani na makafiri wa London ambapo yeye anaishi chini ya hukumu zao pasi na dharurah?

أَكُفَّارُكُمْ خَيْرٌ مِّنْ أُولَـٰئِكُمْ أَمْ لَكُم بَرَاءَةٌ فِي الزُّبُرِ

”Je, makafiri wenu ni bora kuliko hao wa mwanzoni au mna msamaha katika maandiko tukufu?” (54:43)

Hivi kweli mtu huyu haoni hayaa kwa kitendo chake hichi? Au anaingia katika maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ukiwa huna hayaa basi fanya utakalo.”?

Usiwarushie watu mawe ikiwa nyumba yako ni ya vioo.

[2] Kanda inaitwa “Laysa min an-Naswiyhati fiy Shayy´”. Shaykh Muhammad Amaan al-Jaamiy (Rahimahu Allaah) amesema ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

“Sentesi ya mwisho “Kwa ajili hiyo ndio maana vijana wengi wamevipa mgongo na kuvisusa” ni uwongo wenye kukumbushia uwongo wa Ibn Batwuutah juu ya Ibn Taymiyyah ambaye hajapatapo kumuona. Ibn Batwutah alidai kuwa alifika Baghdaad na kumuona Ibn Taymiyyah jinsi anavyoshuka katika minbari huku akisema:

“Allaah huteremka kama ninavyoteremka hivi.”

Allaah akawafanya wanazuoni kuthibitisha uwongo wa kisa hiki kutokana na historia. Bahjah al-Baytwaar akathibitisha katika kitabu chake “Hayaatu Shaykh-il-Islaam” ya kwamba Ibn Batwuutah na Ibn Taymiyyah hawakuwahi kuonana hata siku moja na kwamba Ibn Batwuutah hakupatapo kumuona Ibn Taymiyyah. Wakati Ibn Batwuutah alipofika Baghdaad Ibn Taymiyyah alikuwa gerezani na akafia ndani ya jela. Uwongo huo unaenezwa tu na waandishi.

Uwongo wa leo unahitaji kusambaratishwa na kuraddiwa ili kuitetea ´Aqiydah. Muhammad Suruur si mwenye kustahiki kuamua juu ya kwamba vijana wa Kiislamu ni wenye kuielekea au kuipuuza ´Aqiydah. Sio mwanachuoni. Hakuisoma ´Aqiydah. Haifunzi ´Aqiydah. Ni vipi basi atatoa maamuzi? Ataanzaaje? Ni uzushi tu.

Mmemsikia huyu mchunga Muhammad Suruur akiwakemea majirani zake Hizb-ut-Tahriyr. Ikiwa vitabu vyetu havimtoshelezi, hivi kweli anaweza kuandika kitabu chenye kuvutia na kipya cha Tawhiyd ambacho kitawavutia vijana. Je, alifanya hivi? Lau angelikuwa ni mwanafunzi angefanya hivo. Lakini inavyoonekana ni kuwa mtu huyu – na Allaah ndiye anajua zaidi – ni mwenye chuki dhidi ya Salafiyyah na Salafiyyuun.

Ee Muhammad Suruur! Hivi wewe unalingania katika kitu gani? Mitume waliudhiwa kwa sababu ya kulingania katika Tawhiyd na Uislamu. Wewe unalingania katika kitu gani? Iko wapi ´Aqiydah unayolingania kwayo? Wewe si jengine zaidi ya kwamba ni mpinzani mwenye kuvutana na watawala juu ya kupata uongozi. Ulipoona huna bahati yoyote ndipo ukaanza kutukana, kulaani na kukufurisha. Huu ndio ulinganizi? Unajidai wewe na watu mfano wako kuwa mlinganiaji katika dini ya Allaah. Ulinganio katika dini ya Allaah ni ulinganiaji katika dini Yake, ´Aqiydah na hukumu. Umefanya kitu katika hayo? Hapana.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 75-81
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy