28. Radd kwa wenye kumfanyia Allaah kuwa na watoto

Hii Radd kwa wale waliomthibitishia Allaah kuwa na mtoto ambao ni wafuatao:

1 – Manaswara ambao wamesema kuwa al-Masiyh ni mwana wa Allaah.

2 – Mayahudi ambao wamesema kuwa ´Uzayr ni mwana wa Allaah.

3 – Washirikina ambao wamesema kuwa Malaika ni wasichana wa Allaah. Wamemfanya Allaah kuwa na wasichana ilihali wao wenyewe wanawachukia. Amesema (ta´ala):

وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ مَا يَكْرَهُونَ

“Wanamfanyia Allaah yale wanayoyachukia… “

Wao wenyewe wanawachukia wasichana. Ni vipi basi watamjalia nao Allaah (Jalla wa ´Alaa)? Amesema (Ta´ala):

وَتَصِفُ أَلْسِنَتُهُمُ الْكَذِبَ أَنَّ لَهُمُ الْحُسْنَىٰ

“… na ndimi zao zinaeleza uongo kwamba watapata mema.” (16:62)

Amesema vilevile:

أَمْ لَهُ الْبَنَاتُ

“Au Yeye ana wasichana… “

Mnamfanya Yeye kuwa na wasichana ilihali nyinyi wenyewe mnawachukia.

وَلَكُمُ الْبَنُونَ

“… nanyi mna watoto wa kiume?” (52:39)

Nyinyi wenyewe ndio mnafanya kuwa na wavulana mnaowapenda. Amesema (Ta´ala):

وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ مَا يَكْرَهُونَ وَتَصِفُ أَلْسِنَتُهُمُ الْكَذِبَ أَنَّ لَهُمُ الْحُسْنَىٰ

“Wanamfanyia Allaah yale wanayoyachukia na ndimi zao zinaeleza uongo kwamba watapata mema.” (16:62)

Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَجَعَلُوا لَهُ مِنْ عِبَادِهِ جُزْءًا

“Wakamfanyia kati ya waja Wake sehemu.” (43:15)

Kwa sababu mtoto ni sehemu ya baba. Wao wamemshabihisha Allaah (Jalla wa ´Alaa) na viumbe na wakamfanya kuwa na watoto ilihali Yeye ametakasika kutokana na hayo. Kisha akasema (Jalla wa ´Alaa):

أَوَمَن يُنَشَّأُ فِي الْحِلْيَةِ وَهُوَ فِي الْخِصَامِ غَيْرُ مُبِينٍ

“Hivi kweli yule aliyelelewa katika mapambo naye katika mabishano si mbainifu.” (43:18)

Mwanamke analelewa katika mapambo. Ni mpungufu anahitaji mapambo. Mwanamke ni mpungufu.

وَهُوَ فِي الْخِصَامِ غَيْرُ مُبِينٍ

“… katika mapambo naye katika mabishano si mbainifu.”

Wakati wa mabishano na magomvi mwanamke anadhoofika na wala hayawezi mabishano. Kwa ajili hii mara nyingi mwanamke huwakilisha mtu nafasi hii. Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا

“Wakawafanya Malaika ambao ni waja wa Mwingi wa rehema kuwa ni wa kike.”

Wakasema kuwa ni wasichana wa Allaah.

أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ ۚسَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ

“Je, kwani wao wameshuhudia uumbaji wao?  Utaandikwa ushahidi wao na wataulizwa.” (43:19)

Washirikina wamemsifu Allaah kuwa ana watoto wa kike. Manaswara wamemsifu Allaah kuwa ana mtoto wa kiume ambaye ni al-Masiyh mwana wa Maryam (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Uhakika wa mambo Yeye ni Mtume na mja wa Allaah.

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا

“Akasema: “Hakika mimi ni mja wa Allaah. Amenipa Kitabu na amenijaalia kuwa Nabii.”” (19:30)

إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ

“Yeye si jengine isipokuwa ni mja Tuliyemneemesha na Tukamfanya ni mfano kwa wana wa Israaiyl.” (43:59)

´Iysaa ni mja na Mtume wa Allaah ambaye ni neno Lake alilompelekea Maryam na ni roho.  Kwa hiyo yeye sio mtoto wa Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Subhaanah):

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ

“Hakuzaa na wala hakuzaliwa.” (112:04)

Hakika Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) hana mwanzo kama ambavyo vilevile hana mwisho. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba du´aa na kusema:

“Wewe ndiye wa Kwanza na hakuna kabla Yako kitu na Wewe ndiye wa Mwisho na hakuna kitu baada yako na Wewe ndiye Uliye juu na hakuna juu Yako kitu na Wewe ndiye Uliye karibu zaidi hakuna kilicho karibu zaidi Yako.”[1]

Hizi ndio sifa za Allaah (Jalla wa ´Alaa). Yeye ni wa Kwanza pasi na kuwa na Mwanzo na ni mwenye kudumu pasi na kuwa na mwisho (Subhaanahu wa Ta´ala). Maneno Yake (Ta´ala):

وَلَمْ يُولَدْ

“… na wala hakuzaliwa.”

Haya ni makanusho ya kuwa na washirika na wenye kushabihiana Naye. Mtoto hushabihiana na baba yake na ni mshirika wake. Jengine ni kwamba mtoto anakuwa kwa sababu ya haja ilihali Allaah (Subhaanah) ni mkwasi wa hayo:

هُوَ الْغَنِيُّ ۖ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ

“Yeye ni mkwasi – ni Vyake vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.” (10:68)

Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ni mkwasi kutokana na mtoto. Kuhusu nyinyi ni wenye kuhitajia watoto. Mtu asiyeweza kupata mtoto anakuwa si muweza na ana udhaifu. Ni mwenye kuhitajia mtoto wa kumsaidia. Maneno Yake (Ta´ala):

وَلَمْ يُولَدْ

“… na wala hakuzaliwa.”

Haya ni makanusho.

Maneno Yake (Ta´ala):

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“… na wala hakuna yeyote anayefanana na kulingana Naye.”

Maana yake ni kwamba hana mwenza na mshirika. Allaah (Jalla wa ´Alaa) hana anayeshabihiana Naye wala anayefanana Naye. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna yeyote anayefanana Naye, kuwa sawa Naye na kushabihiana Naye. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.” (42:11)

Huku ni kukanusha washirika na wenza. Amesema (Ta´ala):

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua mwengine anaye jina kama Lake?” (19:65)

Bi maana mnamjua mwengine aliye sawa au ambaye ana jina kama Lake (Subhaanah) kihakika? Haina maana kwamba hakuna yeyote anayeitwa jina Lake kwa mfano mfalme na mtukufu. Maneno ya mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Hana mtoto wala hana baba.”

yamechukuliwa kutoka katika Suurah “al-Ikhlaasw” ambamo ndani yake kuna uthibitisho wa umoja na ukusudiwaji kwa Allaah na kumkanushia mwana na baba na vilevile kumkanushia kushabihiana Naye (Subhaanahu wa Ta´ala). Hashabihiani na yeyote katika viumbe Wake.

[1] Muslim (61) na (2713)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 84-87
  • Imechapishwa: 09/01/2024