Swali 28: Ni ipi hukumu mwanaume na mwanamke kufanya I´tikaaf? Je, I´tikaaf imeshurutisha mtu kufunga? Mwenye kufanya I´tikaaf ajishughulishe na nini? Mwenye kufanya I´tikaaf aanze lini na amalize lini?

Jibu: Kufanya I´tikaaf ni Sunnah kwa wanaume na wanawake. Kutokana na yale yaliyothibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf katika Ramadhaan na mwishoni akawa anafanya I´tikaaf siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Baadhi ya wakeze walikuwa wakifanya I´tikaaf pamoja naye. Kisha baada ya yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufa baadhi ya wakeze wakawa wanafanya I´tikaaf.  I´tikaaf inafanywa misikitini ambapo kunaswaliwa swalah za mkusanyiko. Ikiwa I´tikaaf yake ikiwa na kundi la watu wengine basi bora wafanye I´tikaaf katika msikiti mkubwa wa mji ikiwa kuna urahisi wa kufanya hivo.

I´tikaaf haina wakati maalum kwa mujibu wa maoni yenye nguvu zaidi ya wanachuoni. Wala I´tikaaf haikushurutisha mtu kufunga. Lakini mtu akifunga ndio bora zaidi.

Sunnah yule mwenye kufanya I´tikaaf aanze pale atakaponuia kukaa I´tikaaf na atoke baada ya kumalizika kwa muda aliyonuia kuikata haja ikipelekea kufanya hivo. Kwa sababu kufanya I´tikaaf ni Sunnah na wala si lazima mtu kuianza ikiwa midhali mtu hajaweka nadhiri.

Imependekezwa kufanya I´tikaaf katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan kwa ajili ya kumuigiza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imependekezwa kwa yule mwenye kufanya I´tikaaf kuanza I´tikaaf yake baada ya swalah ya Fajr siku ya tarehe ishirini na moja. Hivo ni kwa kumuigiza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atoke katika I´tikaaf baada ya kumalizika masiku haya kumi. Akiikata hakuna neno juu yake midhali hajaweka nadhiri, kama tulivyotangulia kusema. Bora kwa yule mwenye kufanya I´tikaaf atenge sehemu maalum msikitini ambapo anaweza kupumzika ikiwa ni wepesi kufanya hivo.

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa mwenye kufanya I´tikaaf akithirishe kufanya Dhikr, kusoma Qur-aan, kumuomba Allaah msamaha, kuomb adu´aa na kuswali katika zile nyakati zisizokuwa za makatazo. Hakuna neno akawatembelea baadhi ya marafiki zake na akazungumza nao, kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivokuwa akiwatembelea baadhi ya wakeze na akizungumza nao. Siku moja Swafiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimtembelea wakati alipokuwa amekaaa I´tikaaf katika Ramadhaan. Swafiyyah aliposimama kwenda zake akasimama naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka kwenye mlango wa msikiti. Ni dalili inayoonyesha kuwa hakuna ubaya kufanya hivo. Kitendo chake hichi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinafahamisha juu ya ukamilifu wa unyenyekevu wake, kutangamana kwake kwa wema na wakeze (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake, Maswahabah zake na waliowafuata kwa wema.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdllaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah tata´alaqah bisw-Swiyaam, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 12/05/2019