1- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa matangamano mazuri ni kama muuzaji manukato. Ikiwa hukupata kitu kutoka kwake basi angalau utapata harufu yake. Mfano wa matangamano mabaya ni kama muhunzi. Ikiwa hukupatwa na moto wake basi angalau utapatwa na shari yake.”

2- Mwenye busara anatakiwa kulazimiana kutangamana na watu wema na kujiepusha na kutangamana na waovu. Kuwapenda wema kunafungamana mbiombio na kunachukua muda mrefu kukatika. Kuwapenda waovu kunavunjika mbiombio na kunachukua muda mrefu kufungamana. Kusuhubiana na watu waovu kunapelekea kuwadhania vibaya wema. Yule anayesuhubiana na waovu kuna khatari juu yake kuwa mmoja katika wao.

3- Ni wajibu kwa mwenye busara kujiepusha na watu wenye mashaka ili yeye mwenyewe asiwe ni mtu mwenye mashaka. Kama ambavyo kusuhubiana na watu wema kunapelekea katika kheri kutangamana na watu waovu kunapelekea katika uovu.

4- Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:

“Anayempenda mtu mwema anapenda Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

5- Maalik bin Diynaar amesema:

“Kuyahamisha mawe na watu wema ni bora kuliko kula vitu tamtam na watu waovu.”

6- Mwenye busara haichafui heshima yake na wala haizoezi nafsi yake sababu za shari kwa kusuhubiana na watu waovu. Hafumbii macho kuichunga heshima yake na kujifanyisha mazoezi kwa kutangamana na watu wema.

7- Abu ´Amr bin al-´Alaa´ amesema:

“Sa´iyd bin Jubayr aliniona nikikaa na vijana. Akanambia: “Ni kipi kinachokufanya kukaa na vijana? Kaa na watu wazima.”

8- Abud-Dardaa´ amesema:

“Ni bora kuwa na rafiki mwema kuliko kuwa peke yako. Kuwa peke yako ni bora kuliko kuwa na rafiki mbaya. Ni bora kuzungumza kheri kuliko kunyamaza. Ni bora kunyamaza kuliko kuzungumza vibaya.”

9- Mwenye busara hatangamani na waovu. Kutangamana na mtu muovu ni kipande cha moto kinachopelekea chuki. Mapenzi yake hayako kama yanavyotakiwa na wala hatekelezi ahadi yake.

10- Miongoni mwa furaha ya mtu kuna sifa nne: mke wake anaafikiana naye, watoto wake wanakuwa wema, ndugu zake wema na riziki yake inakuwa katika nchi yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 99-101
  • Imechapishwa: 16/02/2018