28. Mu´attwilah na Mumaththilah wamekusanya kati ya ukanushaji na ufananishaji

Mu´attwilah ni yule anayekanusha kitu katika majina au sifa za Allaah. Kama mfano wa Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah.

Mumaththilah ni yule anayemthibitishia Allaah sifa hali ya kuzifananisha na za viumbe Wake. Kama mfano wa wahenga wa Raafidhwah.

Uhakika wa mambo ni kwamba kila mkanushaji ni mfananishaji na kila mfananishaji ni mkanushaji.

Kuhusu Mu´attwilah ukanushaji wake uko wazi. Kufananisha kwake sifa za Allaah na sifa za viumbe kunakuja kwa njia ya kwamba ameamini kuwa kuthibitisha sifa za Allaah kunapelekea kushabihisha. Matokeo yake hilo likamfanya kukanusha sifa za Allaah akiwa ni mwenye kukimbia hilo. Hivyo akawa ni mwenye kufananisha kwanza kisha ndio akakanusha.

Ama kuhusu Mumaththilah kufananisha kwake kuko wazi. Ama kukanusha kwake kunapatikana kwa njia tatu zifuatazo:

1- Amekanusha andiko linalothibitisha sifa kwa vile ameligeuza kinyume na udhahiri wa linavyofahamisha. Hakika andiko linafahamisha kuthibitisha sifa yenye kulingana na Allaah. Kwa msemo mwingine andiko halifahamishi juu ya kufanana sifa za Allaah na za viumbe Wake.

2- Akimfananisha Allaah na viumbe Wake basi amekanusha maandiko yote yanayojulisha juu ya kukanusha Allaah kufanana na viumbe Wake. Kwa mfano amesema (Ta´ala):

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua mwenye jina kama Lake?” [1]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [na kulingana] Naye.” [2]

3- Akimfananisha Allaah na viumbe Wake basi amemkanushia ukamilifu Wake ambao ni wa wajibu, kwa sababu atakuwa amemshabihisha Mola mkamilifu na viumbe wapungufu kwa njia zote.

[1] 19:65

[2] 112:04

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 74
  • Imechapishwa: 11/05/2020