Salaf (Rahimahumu Allaah) walikuwa hawasikilizi maneno ya wazushi. Walikuwa wakitilia pupa kwelikweli kujitenga mbali na yale maeneo yote ambayo wazushi wanazungumza. Ibn Battwah amepokea katika “al-Ibaanah” kwa cheni ya wapokezi wake kupitia kwa Ma´mar aliyesema:

“Ibn Twaawuus alikuwa ameketi chini. Akaja bwana mmoja katika Mu´tazilah na akaanza kuzungumza. Ibn Twaawuus akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake na akasema kumwambia mtoto wake: “Ee mwanangu! Weka vidole vyako masikioni mwako na uzibe kwa kukaza na usisikize chochote katika maneno yake. Ma´mar akasema: “Hakika ya moyo ni dhaifu.”[1]

Ibn Battwah amepokea tena kupitia kwa ´Abdur-Razzaaq ambaye ameeleza:

“Ibraahiym bin Muhammad bin Abiy Yahyaa alinambia: “Naona Mu´tazilah ni wengi kwenu.” Nikajibu: “Ndio na wanadai kuwa wewe ni mmoja wao.” Akasema: “Si uje na mimi tuingie kwenye duka hili ili nikuzungumzishe?” Nikasema: “Hapana.” Akasema: “Kwa nini?” Nikasema: “Moyo ni dhaifu na dini sio kwa yule mshindi.”[2]

Ibn Battwah amepokea tena kwa cheni ya wapokezi wake kupitia kwa Sa´iyd bin ´Aamir ambaye amesema: Sallaam bin Abiy Mutwiy´ ametuhadithia kwamba kuna bwana mmoja katika wazushi alisema kumwambia Ayyuub as-Sikhtiyaaniy: “Ee Abu Bakr! Nikuulize juu ya neno?” Ayyuub akawa anaashiria kwa vidole vyake: “Sitaki wala nusu ya neno, sitaki wala nusu ya neno.”[3]

Namna hii ndivo walivokuwa Salaf (Rahimahumu Allaah). Walikuwa wanajitenga kuwasikiliza wazushi. Bali walikuwa wakitahadharisha jambo hilo ili moyo usije kuingiwa na kitu katika Bid´ah na hivyo ukaangamia. Wangesemaje juu ya mtu ambaye anaketi na wazushi na anahudhuria darsa zao? Hapana shaka yoyote kwamba maneno yao katika hali hii yangekuwa mabaya na makali zaidi.

[1] ”al-Ibaanah” (02/446).

[2] ”al-Ibaanah” (02/446).

[3] ”al-Ibaanah” (02/447).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 69-70
  • Imechapishwa: 12/11/2020