28. Matunda ya elimu: thawabu zako ukiwa hai na baada ya kufa

8- Miongoni mwa matunda ya elimu ni ule uendeleaji wa thawabu katika uhai na baada ya kufa. Mwanafunzi anapojifunza elimu kisha akaieneza kwa muislamu ambapo muislamu huyu akatendea kazi elimu hii, anakuwa na ujira mkubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Atayejifunza elimu ana ujira wa yule atayaitendea kazi. Hakutopungua kitu katika ujira wa yule mtendaji.”[1]

Mwanafunzi! Pindi utapojifunza Sunnah, faradhi au Dhikr kisha ukamfunza muislamu ambapo muislamu huyo akaja kutendea kazi kitu hicho, basi utakuwa na ujira mfano wa ujira wake. Na muislamu huyo akimfunza mwingine, wewe bado utapata sawa na ujira wa yule mtu mwingine. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah! Ninaapa kwa Allaah ya kwamba hizi ni thawabu na ujira mwingi. Uhakika wa mambo ni kuwa ujira hausimami kwa wewe kufa. Bado utaendelea kupata ujira ilihali umo ndani ya kaburi lako. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Atapofariki mwanaadamu na matendo yake pia hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2] Katika upokezi mwingine imekuja: “Au elimu ni yenye kutendewa kazi baada yake.”[3]

Mwanafunzi! Unatakiwa kupupia kujifunza elimu kisha baada ya hapo upupie kuieneza elimu kati ya watu. Hakika katika kufanya hivo kuna ujira mkubwa. Uhai wako utakatika lakini thawabu zako hazikatiki. Ujira wako utakujia ilihali umo ndani ya kaburi lako. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah! Hakika ni thawabu nyingi kweli!

[1] Ibn Maajah (240). al-Albaaniy amesema katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (01/19):

“Ni Swahiyh kutokana na zengine.”

[2] Muslim (1631)

[3] Ibn Maajah (241) na Ibn Hibbaan (93). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Ta´aliyqaat-ul-Hasaan” (93)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016