Mambo yanayochengua shahaadah mbili. Mambo hayo ndio yale yanayochengua Uislamu. Kwa sababu shahaadah mbili kwa kuzitamka ndizo zinazomwingiza mtu ndani ya Uislamu. Kule kuzitamka mtu anakubali yale yanayofahamishwa nalo na kulazimiana kutekeleza yale yanayopelekea katika kutekeleza nembo za Uislamu. Akiharibu malazimisho haya basi amevunja ahadi aliyoitoa wakati alipotamka. Vichenguzi vya Uislamu ni vingi. Wanachuoni wameviwekea mlango maalum katika vitabu vya Fiqh kwa jina “Mlango kuhusu kuritadi”. Muhimu zaidi ni vile vichenguzi kumi vilivyotajwa na Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) pale aliposema:

1- Shirki katika ´ibaadah ya Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[2]

Kunaingia pia kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah kama wale wanaochinja kwa ajili ya makaburi au kwa ajili ya majini.

2- Atakayeweka baina yake yeye na Allaah wakatikati ambapo anawaomba na anawaomba wamshufaie na akawategemea, amekufuru kwa maafikiano.

3- Yule asiyewakufurisha washirikina [makafiri], akawa na shaka juu ya ukafiri wao au akaona kuwa dini yao ni sahihi, amekufuru.

4- Mwenye kuitakidi ya kwamba uongofu usiyokuwa wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni bora kuliko uongofu wake au ya kwamba hukumu ya asiyekuwa yake ni bora kuliko hukumu yake; kwa mfano kama wale wanaofadhilisha hukumu ya Twawaaghiyt juu ya hukumu yake, huyo ni kafiri.

5- Yule mwenye kuchukia kitu katika yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ijapokuwa atakifanya, amekufuru.

6- Mwenye kufanyia istihzai kitu katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), thawabu yake  au adhabu yake, basi amekufuru. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Hivyo msitoe udhuru, kwani hakika mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[3]

7- Uchawi. Unajumuisha Swarf na ´Atwf. Pengine anakusudia yale yanayofanywa ili mume awe mbali na mke wake au kufanya kitu chenye kufanya mke akavutika kwake. Atakayeufanya au akawa radhi nao amekufuru. Dalili ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

”Na [hao Malaika wawili] hawamfundishi yeyote mpaka wamwambie kwanza: “Hakika sisi ni mtihani, hivyo basi usikufuru [kwa kufanya uchawi].”[4]

8- Kuwasaidia washirikina dhidi ya waislamu. Dalili ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

”Yeyote atakayewafanya vipenzi, basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah haongoi watu madhalimu.”[5]

9- Mwenye kuitakidi ya kwamba baadhi ya watu wana haki ya kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama jinsi Khidhr alivyopata kutoka katika Shari´ah ya Muusa (´alayhis-Salaam), amekufuru.”

Kama wanavyoamini Suufiyyah wachupaji mpaka kwamba wamefikia katika kiwango wasichohitajia kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

10-Kuipuuza dini ya Allaah kwa njia ya kwamba mtu hajifunzi nayo wala haifanyii kazi. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ

”Wale waliokufuru wanapuuza yale wanayoonywa.”[6]

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن ذُكِّرَ بِآيَاتِ رَبِّهِ ثُمَّ أَعْرَضَ عَنْهَا ۚ إِنَّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ مُنتَقِمُونَ

”Na nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa Aayah za Mola wake, kisha akakengeuka nazo? Hakika Sisi Tutawalipiza wahalifu.”[7]

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakuna tofauti katika vichenguzi hivi vya Uislamu kati ya mwenye kufanya mzaha na mwenye kukusudia na mwenye kuogopa isipokuwa tu yule aliyetenzwa nguvu. Na yote haya ni katika mambo makubwa ambayo yanakuwa ni yenye khatari na hutokea mara nyingi. Hivyo basi, inatakikana kwa muislamu kutahadhari navyo na aviogope juu ya nafsi yake. Tunajikinga kwa Allaah dhidi ya yale yanayopelekea katika ghadhabu Zake na adhabu Yake iumizayo.”

[1] 04:48 na 116

[2] 05:72

[3] 09:65-66

[4] 02:102

[5] 05:51

[6] 46:03

[7] 32:22

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 51-53
  • Imechapishwa: 20/02/2020