155- Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Hakika Sisi Tumefanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili Tuwajaribu ni nani miongoni mwao mwenye ‘amali nzuri kabisa.” (18:07)

156- Sufyaan ath-Thawriy amesema:

“´Amali nzuri ni wale wenye kuipa kisogo zaidi dunia.”

Kadhalika ndivyo alivyosema Abu ´Iswaam al-´Asqalaaniy. Kuipa nyongo dunia kwa mujibu wa waarabu maana yake ni kujiepusha na mali na vyeo.

157- Abu Bakr, ´Umar, ´Aliy, Abu Dharr, ´Uthmaan, Abud-Dardaa´, Tamiym ad-Daariy na watu mfano katika Maswahabah walikuwa ni wenye kuipa nyongo dunia. Ni Maswahabah wangapi waliokuwa wanaipa nyongo dunia! ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf na az-Zubayr pia walikuwa ni wenye kuipa nyongo dunia. Upokezi wenye kusema kuwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf atatambaa Peponi upuuzwe. Hakuna atayekuja Peponi kabla yake na hakuna mtu yoyote anaweza kulinganishwa na az-Zubayr.

158- Maalik bin Anas amesema:

“Kuipa nyongo dunia ina maana ya uchamungu.”

159- al-Musayyab bin Waadhwih amesema:

“Sufyaan bin ´Uyaynah aliulizwa juu ya kuipa nyongo dunia ambapo akajibu: “Ina maana ya kujizuia na vile Allaah alivyoharamisha. Kuhusu vile Allaah alivyohalalisha, ni halali. Mtume alikula, akanywa na akaoa.”

161- az-Zuhriy aliulizwa juu ya kuipa nyongo dunia ambapo akajibu:

“Maana yake ni vya haramu visishinde subira yako na vya halali visidhinde shukurani yako.”

162- Sufyaan ath-Thawriy na watu wake wamesema:

“Kuipa nyongo dunia maana yake mtu asiwe na mipango katika mustaqbal.”

Haya ni maneno mazuri, kwa sababu yule asiyekuwa na mipango huko mbeleni ataipa dunia hii mgongo na kumtekelezea ´ibaadah Mola.

163- Ibn Zaraarah bin Awf amesema:

“Kuipa nyongo dunia ni kujitenga mbali na watu.”

Hii ni ishara ya mtu kuwa faragha na kufanya ´ibaadah na kupenda upweke. Abu Sulaymaan al-Khattwaabiy alipatia pale aliposema:

Nafurahi kwa upweke wangu na kukaa nyumbani

uzuri wangu umepatikana na furaha yangu imetimia

Wakati umenifunza na sijali watu wakiniepuka

sitembelei na wala sitembelewi

Maadamu niko hai siulizi

rafiki akishika njia yake au kiongozi akishika kipando chake

164- Ja´far bin Sulaymaan amesema:

“Nilimuuliza mwanamke mwema: “Ni nani yuko nyumbani kwako?” Akajibu: “Yule ambaye ninapata mawasiliano ya karibu Naye. Ee Mja wa Allaah! Ni vipi nitajihisi upweke ilihali Yeye ndiye ninatangamana Naye?”

165- al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Ninapoona usiku umeingia basi hufurahi na kufikiria kuwa nitakuwa faragha na Mola wangu. Ninapoona asubuhi imeingia basi huingiwa na huzuni kwa sababu sitaki kukutana na watu na kuwa na kitu ambacho kitanishughulisha mimi na Mola wangu (´Azza wa Jall).”

166- Kuna mtu alimwambia al-Hasan:

“Wanachuoni wetu wanasema.” al-Hasan akamwambia: “Wewe umemuona mwanachuoni? Mwanachuoni ni yule anayeipa nyongo dunia, ana elimu juu ya dini na ni mwenye kudumu katika kumuabudu Mola wake.”

167- Ibn-ul-Mubaarak amesema:

“Kuipa nyongo dunia ni moyo wa mtu kujiepusha na mambo ya kidunia.”

Haya ni maneno mazuri sana. Ni mamoja mtu akawa na kitu mkononi au asiwe nacho. Hakika kuipa nyongo dunia ni katika matendo ya moyo. Maswahabah walikuwa na dunia yote mikononi mwao pamoja na hivyo walikuwa ni wenye kuipa kisogo dunia kwa mioyo yao.

168- Kuna waliosema kuwa kuipa nyongo dunia ni kupenda umauti. Tafsiri hii inazikusanya tafsiri zengine zote zilizotangulia. Ambaye anapenda umauti anapenda kukutana na Mola wake na kuipa dunia hii mgongo.

169- Shaqiyq amesema:

“Nilinunua tikiti kwa ajili ya mamangu. Nilipolikata akakasirika. Nikamwambia: “Ee mamangu! Umemkasirikia nani? Je, wewe unayarudisha makadirio au unamlaumu mlimaji wake, mnunuzi au Muumbaji? Kuhusu mlimaji na mnunuzi, ninaapa kwa Allaah ya kwamba hawana kosa lolote lolote. Wote walikuwa wakitamani litakuwa tikitiki zuri kabisa. Mimi sioni unamlaumu mwengine isipokuwa Muumbaji wake. Mche Allaah na wala usimlaumu!” Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mamangu hajapatapo kusikia kutoka kwangu maneno yenye manufaa kabisa kama haya.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 102-106
  • Imechapishwa: 18/03/2017