Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

24- Kila kitu ni chenye kumuhitajia Yeye.

MAELEZO

Hakuna chochote kiwezacho kujitosheleza na Allaah. Si Malaika, wala mbingu, wala majini, wala ardhi, wala watu, wala vitu visivyokuwa na uhai kama majibali na bahari. Kila kitu ni chenye kumuhitajia Allaah:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

“Enyi watu!  Nyinyi wote ni mafakiri kwa Allaah na Allaah ndiye Mkwasi,  Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[1]

Kila kitu ni chenye kumuhitajia Yeye, wakiingia mawalii na mbingu. Wako wanaosema kwamba mawalii wana uwezo usiyokuwa wa kibinaadamu ambao kwao ndio wanaendesha walimwengu na kwamba wananufaisha na kudhuru. Hivo ndivo wanavosema makafiri na washirikina. Hakuna katika mawalii, Mitume wala Malaika yeyote awezaye kujitosheleza kutokamana na Allaah. Hakuna yeyote anayeendesha ulimwengu asiyekuwa Allaah. ´Aqiydah hii ndio yenye kutokomeza ´ibaadah kwa asiyekuwa Allaah katika masanamu na vyenginevyo. Ni vipi utaweza kuabudu vitu ambavyo ni vihitaji na fakiri na ukamsahau Ambaye mikononi Mwake ndimo mna ufalme wa kila kitu? Wakati wanachuoni wa waabudu makaburi waliposema kumwambia mtu wa kawaida katika watu wa Tawhiyd kwamba wanasema kuwa mawalii hawadhuru wala hawanufaishi, akalikubali hilo na akanukuu maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ

“ala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Mola wao wanaruzukiwa.”[2]

Je, Allaah amesema kuwa wanaruzuku au wanaruzukiwa? Amesema kuwa wanaruzukiwa. Midhali amesema kuwa wanaruzukiwa basi sisi tunamuomba Yule mwenye kuwaruzuku na hatuwaombi wenye kuruzukiwa. Mwanachuoni yule akasambaratika kutokana na hoja ya kimaumbile ya mtu yule wa kawaida.

[1] 35:15

[2] 03:169

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 19/09/2019