Zipo hukumu za swalah anazopambanuka kwazo mwanamke kutokamana na wanaume. Nazo ni kama zifuatazo:

1 –  Mwanamke hana adhaana wala Iqaamah. Adhaana imewekewa Shari´ah ya kunyanyua sauti na mwanamke haifai kwake kunyanyua sauti na wala viwili hivyo havisihi kwake. Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Hatujui aliyesema kinyume na hivo.”[1]

2 – Mwili wote wa mwanamke ni uchi ndani ya swalah isipokuwa uso wake, viganja vyake vya mikono na kuhusu nyayo zake kuna tofauti. Hali hiyo ni pale ambapo haonekani na mwanaume yeyote ambaye si Mahram yake. Akiwa ni mwenye kuonekana na mwanaume ambaye si Mahram yake basi italazimika kwake kujisitiri kama ilivyo lazima kujisitiri nje ya swalah anapokuwa mbele ya wanaume. Ni lazima ndani ya swalah yake kufunika kichwa chake, shingo yake na kufunika mwili wake mzima mpaka nyayo za miguu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah haikubali swalah ya mwenye hedhi – yaani ambaye kishabaleghe kwa hedhi – isipokuwa kwa Khimaar.”

Wameipokea watano.

Khimaar ni kile kinachofunika kichwa na shingo. Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, mwanamke aswali ndani ya dera lake na Khimaar pasi na shuka ya chini?” Akasema: “Ikiwa dera hilo ni pana linafunika kuonekana kwa nyayo zake.”

Ameipokea Abu Daawuud na maimamu wakaisahihisha pamoja na kwamba ni Mawquuf.

Hadiyth yetu imetufahamisha kwamba ni lazima kufunika kichwa chake na shingo yake ndani ya swalah kama ilivyofidisha pia Hadiyth ya ´Aaishah na kadhalika kufunika mwili wake mzima kusionekane mpaka miguu yake kama ilivyofidisha Hadiyth ya Umm Salamah.

Inafaa kufunua uso wake kwa njia ya kwamba asionekane na mwanaume ajinabi kwa mujibu maafikiano ya wanachuoni juu ya hilo. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Iwapo mwanamke ataswali peke yake basi ameamrishwa kuvaa Khimaar. Nje ya swalah inafaa kwake kufunua kichwa chake nyumbani kwake. Kuvaa mavazi ndani ya swalah ni haki ya Allaah. Haifai kwa yeyote kufanya Twawaaf kwenye Ka´bah akiwa uchi hata kama atakuwa peke yake usiku na wala haifai akaswali uchi hata kama atakuwa peke yake.” Mpaka aliposema: “Kwa hiyo uchi wa ndani ya swalah haikufungamana na uchi wa kutazamwa. Si kwa kukisiwa wala kinyume chake.”[2]

Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Ni lazima kufunika mwili mzima wa mwanamke ambaye ni muungwana. Kukionekana kitu basi haitosihi swalah yake isipokuwa kama itakuwa ni kitu kidogo tu. Hayo ndio maoni ya Maalik, al-Awzaa´iy na ash-Shaafi´iy.”

3 – Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Mwanamke anatakiwa kujikusanya katika Rukuu´ na Sujuud badala ya kujiachia. Vilevile anatakiwa kukaa kikao cha Tarabbu´, atoe mguu wake katika upande wa kulia badala ya kikao cha Tawarruk na Iftiraash. Kwa sababu hivo kunamsitiri zaidi.”[3]

an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´”:

“ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Mukhtaswar”: “Hakuna tofauti kati ya mwanaume na mwanamke katika matendo ya swalah. Isipokuwa tu imependekezwa kwa mwanamke kujikusanya na aambatanishe tumbo lake na mapaja yake katika Sujuud kama inavyositiri zaidi anavokuwa. Napendekeza afanye hivo pia katika Rukuu´ na swalah yote.”[4]

4 – Wanawake kuswali kwa mkusanyiko kwa kuongozwa na mmoja wao ni jambo ambalo wanachuoni wametofautiana kwalo; wako wanaolikataza na wenye kujuzisha. Wengi wanaona kuwa hakuna ubaya kufanya hivo. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha Umm Warqah kuwaongoza katika swalah watu wa nyumbani kwake. Wengine wanaona kuwa imependekezwa kufanya hivo kutokana na Hadiyth hii. Wengine wanaona kuwa haikupendekezwa. Wengine wanaona kuwa imechukizwa. Wengine wanaona kuwa inafaa katika swalah za sunnah pasi na swalah za faradhi. Pengine maoni yenye nguvu ikawa imependekezwa. Kwa faida zaidi rudi katika “al-Mughniy”[5] na “Majmuu´-ul-Fataawaa”[6].

Mwanamke asome kwa sauti midhali hakuna mwanaume ambaye si Mahram yake anayemsikia.

5 – Ni halali kwa wanawake kutoka majumbani kwa ajili ya kwenda kuswali misikitini pamoja na wanaume pamoja na kwamba bora ni kuswali kwao majumbani mwao. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwazuie wajakazi wa Allaah kutokamana na misikiti ya Allaah.”

 “Msiwazuie wanawake kutoka kwenda misikitini – na nyumba zao ni bora kwao.”

Ameipokea Ahmad na Abu Daawuud.

Kwa hiyo kubaki kwao majumbani na kuswali ndani yake ndio bora kwao kwa ajili ya kujisitiri.

[1] (02/68).

[2] (22/113-114).

[3] (02/258).

[4] (03/455).

[5] (02/202).

[6] (04/84-85).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 55-58
  • Imechapishwa: 04/11/2019