72- Kusimama kwenye mlima wa ´Arafah siku ya tarehe nane kwa muda fulani kwa kuchunga mwezi mwandamo usije kuonekana kimakosa.

73- Kuwasha mishumaa mingi usiku wa kuamkia ´Arafah huko Minaa.

74- Kuomba du´aa usiku wa ´Arafah kwa maneno kumi mara elfu moja:

سبحان الذي في السماء عرشه سبحان الذي في الأرض موطئه سبحان الذي في البحر سبيله

“Ametakasika ambaye ´Arshi Yake iko mbinguni. Ametakasika ambaye athari Zake ziko ardhini. Ametakasika ambaye kwenye bahari ndio kuna njia Yake… “

75- Kusafiri katika ile siku ya nane kutoka Makkah kwenda ´Arafah safari ya mara moja.

76- Kusafiri kutokea Minaa kwenda ´Arafah usiku.

77- Kuwasha moto na mishumaa kwenye mlima wa ´Arafah usiku wa ´Arafah.

78- Kuoga kwa ajili ya siku ya ´Arafah.

79- Mtu kusema wakati anapokaribia ´Arafah na akaona mlima wa Rahmah:

سبحان الله والحمد لله ولا إله إلا الله والله أكبر

“Allaah ametakasika. Himdi zote anastahiki Allaah. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Allaah ni mkubwa.”

80- Mtu kwenda kwa kukusudia ´Arafah kabla ya kuingia wakati wa kusimama, ambao ni nusu ya mchana wa ´Arafah.

81- Mtu kusema katika ´Arafah “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” mara mia moja, kusoma Suurah “al-Ikhlaasw” mara mia moja kisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara mia moja na mwisho wake akazidisha:

وعلينا معه

“Na juu yetu pamoja naye.”

82- Kunyamaza siku ya ´Arafah na kuacha kusoma du´aa.

83- Kupanda juu ya mlima wa Rahmah katika ´Arafah.

84- Kuingia kuba lililo katika mlima wa Rahmah ambalo wanaita kuwa ni kuba la Aadam, kuswali ndani yake na kulizunguka kama wanavyoizunguka Nyumba.

85- Kuamini kwamba Allaah (Ta´ala) hushuka jioni ya ´Arafah katika mlima wa Awraq, anapeana mikono na waliopanda vipandwa na anakumbatiana na wenye kutembea.

86- Imamu kutoa Khutbah mbili katika ´Arafah na anazipambanua baina yazo kwa kikao kama inavyofanywa katika swalah ya ijumaa.

87- Kuswali Dhuhr na ´Aswr kabla ya Khutbah.

88- Kutoa adhaana kwa ajili ya Dhuhr na ´Aswr kabla ya Khatwiyb kumaliza Khutbah yake

89- Imamu kuwaambia wakazi wa Makkah baada ya kumaliza swalah:

“Kamilisheni swalah zenu [kwa kuswali Rak´ah nne]. Kwani sisi ni wasafiri.”

90- Kuswali swalah za sunnah baina ya Dhuhr na ´Aswr katika ´Arafah.

91- Kusoma Adhkaar au du´aa maalum katika ´Arafah. Kama mfano wa du´aa ya al-Khidhr (´alayhis-Salaam) ambayo imetajwa katika “al-Ihyaa´”. Mwanzo wake ni kama ifuatavyo:

يا من لا يشغله شأن عن شأن ولا سمع عن سمع

“Ee Ambaye hushughulishwi na kitu kwa ajili ya kitu kingine wala kusikia kwa ajili ya kusikia kingine… “

Baadhi ya du´aa hizo zinafikia kurasa tano tukilinganisha na kitabu chetu hichi.

92- Baadhi ya watu kuondoka kabla ya jua kuzama.

93- Wasiokuwa wasomi wanasema kuwa kusimama ´Arafah siku ya ijumaa ni sawa na hajj sabini na mbili.

94- Kukusanyika usiku wa kuamkia mchana wa ´Arafah misikitini, au sehemu nyingine nje ya mji, kwa ajili ya kuomba du´aa na kumtaja Allaah pamoja na kunyanyua sauti juu sana, khotuba, mashairi na wanawaiga watu wa ´Arafah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 22/07/2018