28. Ashaa´irah wameleta kitu cha ajabu mno


Ashaa´irah wamekuja kwa kitu ambacho ni cha ajabu kuliko maoni ya Jahmiyyah. Wamesema kwamba Qur-aan imegawanyika sehemu mbili:

Mosi: Maana.

Pili: Matamshi.

Kuhusu sehemu ambayo ni ya maana ni maneno ya Allaah. Allaah anasifika kuwa ana maneno – nayo ni ile maana iliyosimama katika nafsi. Hawaonelei kuwa Allaah anazungumza kwa herufu na sauti. Lakini hata hivyo ni maana iliyosimama juu ya nafsi Yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ama matamshi wanasema kuwa yameumbwa. Wanaonelea kuwa ima ni katika maneno ya Jibriyl au ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wameifanya Qur-aan kuwa na sehemu mbili:

Kwanza: Sehemu iliyoumbwa.

Pili: Sehemu ambayo haikuumbwa.

Kwa ajili hiyo hawakuwa pamoja na Ahl-us-Sunnah ambao wanasema kuwa Qur-aan haikuumbwa wala hawakuwa pamoja na Jahmiyyah ambao wanasema kuwa Qur-aan yote imeumbwa. Wao ni wenye kuyumbayumba. Ni kama mfano wa maneno ya manaswara juu ya al-Masiyh pale wanaposema kuwa ni binaadamu na wakati huohuo yeye ndiye Allaah. Wanaonelea kuwa al-Masiyh sehemu moja ni ya uanaadamu na nyingine ya uungu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 68
  • Imechapishwa: 22/01/2018