11 na 12- Kufa kwa kuchomeka au maradhi yanayokuwa kwenye mbavu za mtu. Kuhusu hilo kuna baadhi ya Hadiyth. Hadiyth iliyotangaa zaidi ni ile iliopokelewa na Jaabir bin ´Atiyk kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mashahidi wako saba mbali na kufa katika njia ya Allaah: kufa kwa maradhi ya tauni ni shahidi, aliyekufa kwa kuzama ni shahidi, aliyekufa kwa maradhi ya kwenye mbavu ni shahidi, aliyekufa kwa maradhi ya tumbo ni shahidi, aliyekufa kwa kuungua moto ni shahidi, aliyekufa kwa kuangukiwa na jengo ni shahidi na mwanamke mwenye kufa kwa Jum´[1] ni shahidi.”

Ameipokea Maalik (01/232-233), Abu Daawuud (02/26), an-Nasaa´iy (01/261), Ibn Maajah (02/185-186), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake (1616- al-Mawaarid), al-Haakim (01/352) na Ahmad (05/446). al-Haakim amesema:

“Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.”

Mimi sina shaka juu ya usahihi wa matini yake. Kwa sababu zipo Hadiyth nyingi zinazoishuhudilia. Zimetangulia nyingi yazo. at-Twabaraaniy amepokea mfano wake kupitia kwa Rabiy´ al-Answaariy hali ya kuirufaisha pasi na kutaja kuangukiwa na jengo. al-Mundhiriy na akafuatwa kwa hilo na al-Haythami (05/300):

“Wapokezi wake wanajengewa hoja katika Swahiyh.”

Ameipokea Ahmad (04/157) kupitia kwa ´Utbah bin ´Aamir hali ya kuirufaisha kwa tamko:

“Kufa kwa maradhi ya mbavuni ni shahidi.”

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri katika shawaahid. Jumla hii imekuja katika baadhi ya njia za Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia katika “alama ya tano.” Ameipokea Ahmad (02/441-442). Ndani yake yumo Muhammad bin Ishaaq ambaye ni mudalisi na ameitaja kwa mtindo wa “kutoka kwa fulani, kutoka kwa fulani”. Pia Hadiyth ya Jaabir bin ´Atiyk iliyopita punde kidogo.

[1] Imekuja katika ”an-Nihaayah:

”Amekufa na mtoto tumboni mwake, imesemekana vilevile kwamba amekufa akiwa bikira kwa umbile lake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 04/02/2020