28. Ahl-us-Sunnah ni wenye kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah katika kila zama na pahala


Swali 28: Ee Shaykh! Allaah akuwafikishe kwa kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah. Lakini hata hivyo baadhi ya Mashaykh hawaonelei kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah na wanasema kuwa sio katika mfumo wa Salaf na kwamba waislamu wote wanashuhudia kuwa hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Wanasema kuwa wote ni waislamu na haijuzu baadhi wakawapiga radd wengine na kwamba wote wanafuata mfumo mmoja. Tunataraji utaondosha utata huu kwa dalili ili jambo hili lisije kuwadanganya baadhi ya wanafunzi walio na elimu changa.

Jibu: Maneno haya ni ya batili. Haijuzu kuyatendea kazi. Bali ni wajibu kwa wanachuoni kumraddi yule mwenye kwenda kinyume na njia ya Kishari´ah na khaswa ikiwa mukhalifu huyu ameenda kinyume katika jambo la ´Aqiydah. Katika hali hiyo ni wajibu kwa wanachuoni kubainisha hilo na waondoshe utata huo na warekebishe uelewa wa kimakosa. Ni wajibu kwa anayejua ambainishie asiyejua. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Waulizeni wenye Ukumbusho ikiwa hamjui.” (16:43)

Kuna mtu alipatwa na donda vitani na usiku ulikuwa na baridi kwelikweli. Akahisi maumivu. Akawauliza wenzake kama anaweza kuwa na udhuru wowote ambapo wenzake wakamkatalia. Matokeo yake akaoga na akafariki. Katika Hadiyth – pamoja na kuwa Hadiyth hii kuna maneno juu yake – ikaja:

“Wamemuua Naye Allaah awaue. Kwa nini hawakuuliza pale walipokuwa hawajui? Dawa ya asiyejua ni kuuliza. Ilitosheleza kwake kupangusa juu ya donda lake.”

Allaah amewaraddi Ahl-ul-Baatwil katika Qur-aan. Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewaraddi katika Sunnah. Vivyo hivyo ndivyo walivyofanya Maswahabah, Taabi´uun na waliokuja baada yao. Kumeandikwa vitabu vikiwaraddi. Vitabu hivyo vya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah havihesabiki. Kwa mfano vitabu vya Imaam Ahmad, Ibn Khuzaymah, ´Uthmaan bin Sa´iyd ad-Daarimiy na wengineo. Bado Ahl-us-Sunnah ni wenye kuendelea kuraddi mpaka ilipofika wakati wa Shaykh Ahmad Ibn Taymiyyah na Ibn-ul-Qayyim. Waliraddi radd nyingi kwelikweli haziwezi kuhesabikiwa isipokuwa kwa utatizi. Kadhalika katika wakati wa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, wenzake na wanafunzi wake. Bado Ahl-us-Sunnah ni wenye kuendelea kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah katika kila zama na mahala.

Aliyesema haya ima ni mjinga mwenye kujiona au ametiwa mchanga wa machoni.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa al-Jaliyyah
  • Imechapishwa: 23/07/2017