27. Uwajibu wa kuhakikisha kwanza kabla ya Tabdiy´ Tafsiyq na Takfiyr

Swali 27: Watu wengi hawahakikishi katika suala la Tabdiy´ na Tafsiyq. Bali wanawahukumu watu kwa dhana. Matokeo yake kunatokea mgawanyiko kati ya Ummah wa Kiislamu kama mambo yalivo hii leo. Una maelekezo yoyote juu ya mtu kuhakikisha katika suala hili la Tabdiy´, Tafsiyq na Takfiyr na kwamba wanatakiwa kurejea kwa wanachuoni wa nchi hii?

Jibu: Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba ni wajibu kwa mtu kuhakikisha kwanza katika jambo hili. Neno hili ni lazima upate ubainifu wake kwanza na utambue kuwa utaulizwa juu yalo mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Kila anayezungumza juu ya watu ni lazima aseme kitu alicho na uhakika kwacho na isiwe kwa dhana. Kuhusu mtu aliyenyamaza haisemwi kuwa yuko katika watu hawa wala hawa. Mtu anatambulika kuwa ni katika Ahl-us-Sunnah na kwamba anafuata mfuomo wa Salafiyyah kwa yeye kupita juu ya mfumo huu na kuwapenda watu wake na kuwa chini ya bendera yake.

Huenda kukawepo watu wenye kudanganyika na watu katika Ahl-ul-Bid´ah wanaodhihirisha wema. Lakini hata hivyo nyuma ya wema huu kukawepo kitu chenye kujificha kisichojulikana na watu wengi. Mtu kama huyu yachukuliwa maneno ya yule anayemtambua midhali mtu huyo ni mwaminifu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipowapa mateka viongozi wa makabila ngamia mia moja na akawapa tena ngamia khamsini alikuja mtu na akamwambia:

“Mgawanyo huu haukukusudiwa ndani yake Uso wa Allaah.”

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hivi kweli hamniamini ilihali naaminiwa na Aliye mbinguni?”

Anakusudia Allaah amemuamini juu ya walioko ardhini ndio maana akawa amenituma kwenu na kunifanya kuwa Mtume wenu. Vipi wewe usiniamini kwa sababu ya kitu tu cha kidunia? Swahabah mmoja akasimama na kuomba amkate kichwa mnafiki yule. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“[Mwache] huenda anaswali.” Swahabah yule akasema: “Ni wangapi wanaoswali ilihali hakuna kheri ndani yao?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika kupitia mtu huyu watajitokeza watu ambao mtazidharau swalah zenu kwa swalah zao, swawm zenu kwa swawm zao na kisimo chenu kwa kisomo chao. Wanatoka katika dini kama jinsi mshale unavotoka kwenye upinde wake.”

Katika upokezi mwingine amesema:

“Twuubaa kwa yule mwenye kuwaua au waliyemuua.”

Katika upokezi mwingine amesema:

“Wao ni mijibwa ya Motoni.”

Pamoja na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa watazidharau – yaani Maswahabah – swalah zao wakilinganisha na swalah zao – yaani za Khawaarij. Wale walioenda maskani kwa Khawaarij walikuwa wakisikia vilio vyao kama kilio cha ngamia. Kutokana na wingi wa swalah zao magoti yao yanakuwa kama nundu ya ngamia. Lakini pamoja na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yao ya kwamba wao ni mijibwa ya Motoni. Ni kwa nini? Ni kwa sababu wamewakufurisha waislamu, wanaonelea kufaa kuwafanyia uasi viongozi, wamewawajibishia kuingia Motoni milele watenda madhambi na wameikataa Sunnah. Maoni haya mane ndio waliyowafanya kustahiki matishio haya. Kwa hivyo usidanganyike na udhahiri wa mtu.

Ni jambo lisilo na shaka ya kwamba tunasema kuwa udhahiri wa mtu ni mzuri midhali hatujui shari kutoka kwake. Pale tutapoambiwa kuwa mtu huyu ameficha kitu kadhaa basi ni wajibu kuchukua maneno ya huyu aliyetwambia endapo atakuwa ni mtu mwaminifu. Wanachuoni wanaposema kuwa watu fulani ni wazushi hawasemi hivo kwa kubahatisha. Wanakuwa wamesema hivo kwa mategemezi ima kwa kukubali kwao wenyewe au kupitia maneno yao. Tatizo ni kwamba Khawaarij wa zama hizi wanaafikiana na Khawaarij wa hapo kale katika kuwakufurisha watu walio na madhambi makubwa na kuwafanyia uasi viongozi. Wanaafikiana nao katika hayo kwa kujifichaficha na wanajifanya kuyapinga kwa dhahiri. Pamoja na kuwa wanapanga mipango ya kuwafanyia uasi watawala pale wanapopata fursa ya kufanya hivo.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa al-Jaliyyah
  • Imechapishwa: 23/07/2017