Ee mwanamke wa Kiislamu! Ichunge swalah yako kwa kuitekeleza katika nyakati zake hali ya kutimiza sharti zake, nguzo zake na mambo yake ya wajibu. Allaah (Ta´ala) anasema kuwaambia kina mama wa waumini:

وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah na mtiini Allaah na Mtume Wake.”[1]

Haya ni maamrisho kuwaelekea wanawake wa kiumini wote. Swalah ndio nguzo ya pili miongoni mwa nguzo za Uislamu. Swalah ndio nguzo ya Uislamu. Kuiacha ni ukafiri unaomtoa mtu nje ya Uislamu. Hakuna dini wala Uislamu kwa yule asiyeswali. Ni mamoja akawa mwanaume au mwanamke.

Kuchelewesha swalah kutoka ndani ya wakati wake pasi na udhuru wa Kishari´ah ni kuipoteza swalah. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا إِلَّا مَن تَابَ

“Wakafuata baada yao waovu walipoteza swalah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu Motoni. Isipokuwa yule aliyetubu.”[2]

Haafidhw Ibn Kathiyr ametaja katika “Tafsiyr” yake kutoka kwa maimamu wengi wenye kufasiri Qur-aan kwamba maana ya “kuipoteza swalah” ni kule kupoteza nyakati zake kwa njia ya kwamba mtu akaswali baada ya kuisha wakati wake. Pia “al-Ghayyaa” imefasiriwa kwamba ni ile khasara watayokuja kukutana nayo na pia wengine wakasema ni bonde lilioko Motoni.

[1] 33:33

[2] 19:59-60

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 55
  • Imechapishwa: 04/11/2019