27. Sunnah katika walima


25- Sunnah katika walima

Yafuatayo yanatakiwa kuzingatiwa:

1- Ifanyike siku tatu tokea siku ile aliyomwingilia kwa sababu hili ndilo lililonukuliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofunga ndoa na mwanamke, akanituma kuwaalika wanaume katika chakula.”[1]

Amesimulia tena huyohuyo:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuoa Swafiyyah na kule kumwacha huru ndio ikawa mahari yake na alifanya walima siku tatu.”[2]

2- Mtu akawaalika watu wema kwenye chakula hicho. Ni mamoja wakawa mafukara au matajiri. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Usisuhubiane isipokuwa na muumini na wala asile chakula chako isipokuwa mchaji.”[3]

3- Achinje kondoo au zaidi ya hivo akiwa na wasaa kutokana na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“´Abdur-Rahmaan bin ´Awf alifika al-Madiynah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amejenga udugu kati yake yeye na Sa´d bin ar-Rabiy´ al-Answaariy. Sa´d akamchukua na kwenda naye nyumbani kwake ambapo akaitisha chakula wakala pamoja. Sa´d akamwambia: “Ee ndugu yangu! Mimi ni mtu ambaye nina mali zaidi hapa al-Madiyah… “ Katika upokezi mwingine imekuja: “… ni Answaariy ambaye nina mali zaidi. Hivyo tazama nusu ya mali yangu uchukue.” Katika upokezi mwingine imekuja: “Twende kwenye bustani yangu na nitakukatia nusu yake na twende kwa wake zangu wawili utazame ni yupi kati yao anayekupendeza zaidi kisha uniache nimtaliki kwa ajili yako, kwa kuwa wewe ni ndugu yangu kwa ajili ya Allaah na huna mke.” ´Abdur-Rahmaan akasema: “Hapana, kwa jina la Allaah! Allaah akubariki wewe na kwenye mali yako. Nielekeze sokoni ambapo akaelekezwa! Akaenda, akauza na akapata faida. Ilipofika jioni, akaja kwa watu wa nyumbani kwake akiwa na maziwa makavu ya kupikia na samli. Akavaa yale apendayo kuvaa. Akajitokeza siku moja akiwa na alama za zaafarani katika nguo zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nini haya?” Akajibu: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeoa mwanamke katika wanawake wa Answaar.” Akasema: “Umempa nini?” Akasema: “Umempa mahari kitu gani?” Akajibu: “Dhahabu ya uzito wa dirhamu tano.” Akasema: “Allaah akubariki. Fanya karamu ijapokuwa kondoo mmoja.” ´Abdur-Rahmaan akasema: “Nilijiona lau ninyanyue jiwe lolote ili niweze kupata chini yake dhahabu au fedha.” Anas amesema: “Nilimuona kila mke wake akirthi dinari laki moja baada ya kufa kwake.”[4]

Anas amesimulia tena:

“Sijapatapo kumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimfanyia karamu kubwa ya ndoa kwa wake zake kama alivyofanya kwa Zaynab; alichinja kondoo mmoja na akawalisha mikate na nyama mpaka wakashiba.”[5]

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (09/189-194), al-Bayhaqiy (07/260) na matamshi ni yake na wengineo.

[2] Ameipokea Abu Ya´laa kwa mlolongo wa wapokezi mzuri kama ilivyo katika “al-Fath” (09/199) na inapatikana katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy (07/387) ikiwa na maana kama hiyo. Matamshi yake yanayokaribiana yatakuja katika masuala ya 26.

[3] Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmdhiy, al-Haakim (04/128) na Ahmad (03/38). al-Haakim amesema:

“Mlolongo wake ni Swahiyh” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[4] Ameipokea al-Bukhaariy (04/232), an-Nasaa´iy (02/93), Ibn Sa´d (03/02/77), all-Bayhaqiy (07/258), Ahmad (03/165) na wengineo.

[5] Ameipokea al-Bukhaariy (07/192), Muslim (04/149) na matamshi na nyongeza ni yake, Abu Daawuud (02/137), Ibn Kaajahu (01/590), Ahmad (03/98) na nyongeza ni yake pia katika upokezi mwingine.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 145-150
  • Imechapishwa: 21/03/2018