27. Mlango kuhusu kuagua na kuondosha uchawi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu kuagua uchawi kwa uchawi ambapo akasema:

“Ni katika matendo ya shaytwaan.”[1]

Ameipokea Ahmad kwa cheni ya wapokezi nzuri na Abu Daawuud ambaye amesema:

“Ahmad aliulizwa kuhusiana na hilo ambapo akasema:

“Ibn Mas´uud anachukia yote haya.”

2- al-Bukhaariy amepokea kwamba Qataadah amesema:

“Nilimwambia Ibn al-Musayyab kuhusu mtu ambaye karogwa au anasumbuliwa juu ya mke wake, je, ni halali kwake kuaguliwa?” Akajibu: “Hakuna neno. Hakika wamechokusudia ni kutengeneza. Kuhusu yanayonufaisha hayakukatazwa.”

3- Imepokelewa kwamba al-Hasan amesema:

“Haufungui uchawi isipokuwa mchawi.”

4- Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“an-Nushrah ni kuondosha uchawi kwa yule aliyefanyiwa uchawi. Kuna aina mbili:

1- Kuuondosha uchawi kwa kutumia uchawi mwingine. Hili ndio katika matendo ya shaytwaan na ndivyo yanavyotakiwa kufahamika maneno ya al-Hasan. Mchawi na anayefanyiwa uchawi wote wawili wanajikurubisha kwa shaytwaan kwa wanayoyataka. Hivyo shaytwaan anamuondoshea aliyerogwa athari za uchawi.

2- Kuuondosha uchawi kwa Ruqyah, du´aa za kinga na dawa zilizoruhusiwa. Hili linajuzu.

MAELEZO

1- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu kuagua uchawi kwa uchawi ambapo akasema:

“Ni katika matendo ya shaytwaan.”

Ni dalili inayothibitisha kwamba uondoshaji au uaguaji wa uchawi unaotambulika katika kipindi cha kikafiri umekatazwa kwa sababu imetajwa katika fomu ya uhakika. Katika kipindi hicho walikuwa wakiondosha na kuagua uchawi kwa kutumia uchawi mwingine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni katika matendo ya shaytwaan.”

Kwa sababu mchawi anajikurubisha kwa mashaytwaan kwa yale wanayoyataka kama kuwaabudu na kuwawekea nadhiri. Matokeo yake ndipo wanawaitikia maombi yao kuhusu matendo ya mchawi na yale aliyomfanyia yule aliyerogwa ambayo yamefichikana kwao. Ni katika matendo ya shaytwaan. Ahmad aliulizwa kuhusiana na hilo ambapo akasema:

“Ibn Mas´uud anachukia yote haya.”

Bi maana uaguzi ambao ni katika matendo ya shaytwaan na ambao ndani yake kuna kujikurubisha kwao.

2- al-Bukhaariy amepokea kwamba Qataadah amesema:

“Nilimwambia Ibn al-Musayyab kuhusu mtu ambaye karogwa au anasumbuliwa juu ya mke wake, je, ni halali kwake kuaguliwa?” Akajibu: “Hakuna neno. Hakika wamechokusudia ni kutengeneza. Kuhusu yanayonufaisha hayakukatazwa.”

Maneno haya yanatakiwa kusafiriwa kwamba ni kule kuondosha na kuagua uchawi kwa njia iliyoruhusiwa kwa kutumia Ruqyah, du´aa za kinga na dawa zilizoruhusiwa. Kwa sababu huku ni katika kutengeneza na kutengeneza ni jambo limeamrishwa na maovu yamekatazwa.

3- Imepokelewa kwamba al-Hasan amesema:

“Haufungui uchawi isipokuwa mchawi.”

Hakuna aondoshaye uchawi kwa njia ya kishaytwaan isipokuwa mchawi. Ama kuhusu kuondosha na kuagua uchawi kwa njia inayokubalika katika Shari´ah ni jambo linaloruhusiwa na wanachuoni, wenye uoni wa mbali na wenye uzowefu. Kwa mfano mtu anaweza kusoma al-Faatihah, Aayah ya al-Kursiy au zote mbili pamoja vilevile na kusoma zile Aayah za uchawi katika Suurah “al-A´raaf”, “Twaahaa”, “Yuunus”, “al-Kaafiruun”, “al-Falaq” na “an-Naas” kwa kurudiarudia akasomewa yule aliyerogwa na mke wake na kuwatemea cheche za mate wakati wa kisomo. Ruqyah hii imetumiwa na wanachuoni na Allaah amenufaisha kwayo.

Hapo kale walikuwa wakichukua majani kutoka katika mti wa kijani wa mkunazi, wakayakunjakunja na kuyaweka ndani ya maji. Baadaye Aayah hizi zikasomwa ndani ya maji hayo na baadaye akayanywa yule aliyefanyiwa uchawi mara tatu halafu akayaoga yale ya kubaki. Matokeo yake akapona yule aliyerogwa. Uaguaji na uondoshaji wa uchawi wa sampuli hii ni wenye kukubalika Kishari´ah na ni dawa zilizoruhusiwa na zilizojaribiwa ambazo hazina makatazo yoyote, si za najisi, ndani yake hakuna kuwakata msaada mashaytwaan wala mambo mengine aliyoharamisha Allaah. Hii ni haki na ni sawa.

4- Ibn al-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“an-Nushrah ni kuondosha uchawi kwa yule aliyefanyiwa uchawi. Kuna aina mbili:

1- Kuuondosha uchawi kwa kutumia uchawi mwingine. Hili ndio katika matendo ya shaytwaan na ndivyo yanavyotakiwa kufahamika maneno ya al-Hasan. Mchawi na anayefanyiwa uchawi wote wawili wanajikurubisha kwa shaytwaan kwa wanayoyataka. Hivyo shaytwaan anamuondoshea aliyerogwa athari za uchawi.

2- Kuuondosha uchawi kwa Ruqyah, du´aa za kinga na dawa zilizoruhusiwa. Hili linajuzu.

Haya yamekwishatangulia.

[1] Abu Daawuud (3868), Ahmad (141667), al-Haakim (8292) na al-Bayhaqiy (19397). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (4553).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 96-98
  • Imechapishwa: 16/10/2018