27. Malengo ya waanzilishi wa imani kwamba Qur-aan sio maneno ya Allaah

Qur-aan hiyo ambayo ndio dalili ya kwanza. Dalili ya kwanza kutegemewa ni Qur-aan, kisha Sunnah kisha maafikiano (Ijmaa´) kisha kipimo (Qiyaas). Kwa hiyo kukisemwa kwamba hakuna Qur-aan kati ya watu, watu watatumia dalili kwa kitu gani? Kukibatilishwa msingi wa kwanza basi kutabatilishwa misingi mingine iliyobaki. Matokeo yake Uislamu utatokomezwa kwa njia hii. Utata wao ni kwamba wanasema eti wanamtakasa Allaah na kuzungumza. Wanaona kuwa wakimsifia kuwa anazungumza wanamfananisha na viumbe. Kwa hiyo ndio maana eti wanamtakasa na jambo hilo. Wamekuja kwa njia ya kutakasa kwa madai yao. Uhakika wa mambo ni kwamba wamekimbia jambo la kufananisha – kama wanavodai – wakatumbukia katika kufananisha ambako ni kubaya zaidi. Wakimkanushia maneno ili wasije kumfananisha na viumbe wanaozungumza wamemfananisha na viumbe visivyokuwa na uhai ambavyo havizungumzi, jambo ambalo ndio upungufu mkubwa. Kwa ajili hiyo maimamu wa Ahl-us-Sunnah wamewahukumu Jahmiyyah kuwa ni makafiri. Imaam Ibn-ul-Qayyim amesema[1]:

Wamewakufurisha khamsini

ndani ya kumi katika wanachuoni wa miji mbalimbali

Khamsini ndani ya kumi bi maana wanachuoni mia tano wamehukumu kuwa Jahmiyyah ni makafiri. Kwa sababu wamekanusha maneno ya Allaah (Subhaanah).

Kwa ajili hiyo Khaalid bin ´Abdillaah al-Qasriy alimuua al-Ja´d bin Dirham kwa sababu ya masuala haya katika siku ya ´Iyd-ul-Adhwhaa. Alisema:

“Enyi watu! Chinjeni! Allaah akubali vichinjwa vyenu. Mimi namchinja al-Ja´d bin Dirham. Anadai kwamba Allaah hakuzungumza na Muusa maneno ya kihakika na wala hakumfanya Ibraahiym kuwa kipenzi wa karibu.”

Kisha akashuka na akamchinja chini ya mimbari mbele ya umati wa wanachuoni na waislamu na wakamshukuru kwa jambo hilo[2]. Kwa ajili hiyo imaam Ibn-ul-Qayyim amesema[3]:

“Kwa ajili hiyo Khaalid bin al-Qasriy akamchinja al-Ja´d siku ya kuchinja. Alifanya hivo kwa sababu alikuwa haonelei kuwa Ibraahiym ni kipenzi cha karibu cha Allaah na wala hakuzungumza na Muusa maneno ya kihakika. Kila mwenye kufuata Sunnah akamshukuru kwa kichinjwa.”

[1]  Tazama ”an-Nuuniyyah” pamoja na maelezo yake ya Ahmad bin ´Iysaa (01/290).

[2] Tazama ”Manhaj-is-Sunnah an-Nabawiyyah” (01/ 309).

[3] Tazama ”an-Nuuniyyah” pamoja na maelezo yake ya Ahmad bin ´Iysaa (01/50).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 47-49
  • Imechapishwa: 15/03/2021