151- ´Abdullaah bin Salaam alikutana na Ka´b-ul-Ahbaar kwa ´Umar bin al-Khattwaab akamwambia:

“Ee Ka´b! Ni wepi mabwana wa elimu?” Akasema: “Ni wale wanaoitendea kazi.” Akamuuliza: “Ni kipi chenye kufanya elimu ikapotea katika vifua vya wanachuoni baada ya kuihifadhi na kuijua?” Akajibu: “Tamaa, nafsi ovu na kuwaomba watu misada.” Akasema: “Umesema kweli.”

152- Sa´d bin Abiy Waqqaas alisema kumwambia wanawe:

“Ee mwanangu! Ukiomba utajiri basi ombe vilevile kukinaika nao. Ukinaifu ni utajiri usiyopotea. Ninakuonya kuwa na tamaa. Tamaa ni ufakiri uliopo. Kata tamaa kwa vile vilivyomo kwenye mikono ya watu. Hakuna kitu ambacho utakikatia tamaa isipokuwa Allaah atakutosheleza nazo.”

153- Abu Ayyuub amesema:

“Kuna mtu alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Nifunze na ufanye fupi.” Akasema: “Unaposimama kwa ajili ya kuswali basi swalah kama vile ni swalah ya mwisho. Usizungumze kwa maneno ambayo utakuja kutaka udhuru kwayo baadae na kata tamaa kwa vile vilivyomo kwenye mikono ya watu.”[1]

154- Imepokelewa namna ambavyo kuna mtawala alimtumia kitu ´Abdur-Rahmaan al-A´raj ambapo akakirudisha. Yule mtawala akamwambia:

“Ni kwa nini umerudisha zawadi yetu ilihali tumefikiwa na khabari kuwa katika mji wako hakuna masikini kama wewe?” Akajibu: “Si kweli. Ni vipi nitakuwa masikini na mimi nina mali mbili ninazoishi kwazo?” Akauliza: “Ni zipi hizo?” Akaseama: “Ya kwanza ni kuridhia kwangu kwa yale niliyopewa na ya pili ni kule kutokuwa kwangu na tamaa na vile vilivyomo kwenye mikono ya watu.”

[1] Ibn Maajah (4171).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 99-100
  • Imechapishwa: 18/03/2017