7 – Kuosha maiti

Hichi ni kichenguzi cha saba miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Ni lazima kwa ambaye ameosha maiti kutawadha tena. Abu Huryarah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuosha maiti basi atawadhe na yule mwenye kubeba maiti atawadhe.”[1]

Hata hivyo ni Hadiyth dhaifu. Ufupisho wake ni kwamba ni dhaifu kusema kwamba ni yenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni Swahiyh kutoka kwa mmoja katika Swahabah[2].

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amefuata madhehebu ya Hanaabilah juu ya kwamba kumuosha maiti kunachengua wudhuu´[3]. Maoni sahihi ni kwamba hakuchengui wudhuu´. Kwa sababu hakuna dalili juu ya ulazima wa kufanya hivo. Lakini hata hivyo imependekezwa. Pengine hekima ya kufanya hivo ni kuwa mtu anapoosha maiti basi anapatwa na baadhi ya taathira. Kwa hiyo kutawadha au kuoga baada ya hapo kunaupa mwili uchangamfu, nguvu na kunamuunga kutokana na yale yaliyompitikia.

Dalili ya kwamba kumuosha maiti hakuwajibishi kutawadha ni kwamba wakati ambapo Asmaa´ bint Umays alimuosha Abu Bakr as-Swiddiyq wakati alipofariki halafu akatoka nje na kuwauliza baadhi Maswahabah wa Makkah waliokuweko pale: “Mimi nimefunga na hii leo kuna baridi kali. Je, nalazimika kuoga?” Wakamjibu: “Hapana.”[4]

8 – Kuritadi kutoka katika Uislamu – Tunamuomba Allaah Atukinge na hilo

Hichi ni kichenguzi cha nane miongoni mwa vichenguzi vya wudhuu´. Amesema (Ta´ala):

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ

“Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako.”[5]

Twahara ni moja katika matendo[6].

[1] Abu Daawuud (3161), at-Tirmidhiy (993), Ibn Maajah (1463) na Ahmad (02/272).

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ya Abu Hurayrah ni nzuri. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah ikiwa na cheni ya wapokezi pungufu.”

[2] Tazama ”al-Badr-um-Muniyr” (02/526-529).

[3] Tazama ”al-Mughniy” (01/123).

[4] ”al-Muwattwa´” (521) ya Maalik.

[5] 39:65

[6] Tazama ”al-Mughniy” (01/115).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 38-40
  • Imechapishwa: 29/12/2021