Ndugu wapendwa! Tumekwishatangulia katika kikao cha tatu kwamba kufaradhishwa kwa funga kulikuwa katika ngazi mbili kisha baadaye kukathibiti hukumu ya kufunga. Watu walikuwa wamegawanyika mafungu kumi:

1-  Muislamu, ambaye kishabaleghe, kishapata akili, mkazi, muweza ambaye amesalimika kutokamana na vikwazo. Muislamu kama huyu ni lazima kwake kufunga Ramadhaan aitekeleze ndani ya wakati wake kutokana na dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano juu ya hilo. Allaah (Ta´ala) amesema:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ َ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[1]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtapoona mwezi mwandamo basi fungeni.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Waislamu wameafikiana juu ya ulazima wa kufunga kwa yule ambaye punde tumemweleza.

Kuhusu makafiri si lazima kwao kufunga na wala haisihi kutoka kwao kwa sababu si wenye kustahiki kufanya ´ibaadah. Kafiri akisilimu katikati ya mwezi wa Ramadhaan basi si lazima kwake kulipa siku zilizompita. Amesema (Ta´ala):

قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ

“Waambie wale waliokufuru kwamba wakikoma watasamehewa yaliyotangulia.”[2]

Akisilimu katikati ya siku ya Ramadhaan basi ni lazima kwake kujizuia siku iliobaki. Kwa sababu  amekuwa miongoni mwa watu waliowajibika kuanzia pale aliposilimu na wala si lazima kuilipa siku hiyo. Kwa sababu hakuwa miongoni mwa watu wanaowajibika kufunga pale alipojizuia.

[1] 02:185

[2] 08:38

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 21/04/2020