27. Bainisha haki na usijadiliane na mtu wa Bid´ah

Kuamini Mizani na kwamba matendo yatapimwa, madaftari na yule mtendaji ni miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hawajadili juu ya hilo. Hawashiki msimamo wa kunyamaza wala hawapindishi maana. Wanayaamini maandiko haya kama yalivyokuja kutoka kwa Allaah na Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam). Jukumu lao ni kubainisha, na sio kujadili, kugombana na kuzozana. Kuwabainishia watu ndio jukumu walilokuwa nalo Mitume na Manabii. Wanachuoni, ambao ndio warithi wao, wanabainisha. Mijadala na magomvi sio katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah. Hayo ni mambo ya wale waliopewa mtihani. Salaf na wafuasi wao walitahadharisha juu ya mijadala na mizozo.

Hii leo ni lazima kwetu kulitia hilo manani. Tukiwaona Ahl-ul-Bid´ah anajadili, anatetea Bid´ah na hakubali nasaha na maelekezo, basi anaachwa. Wanafunzi wa Ahl-us-Sunnah hawatakiwi kuleta mivutano nao isiyokuwa na faida yoyote. Kama Allaah anawatakia watu hawa kheri basi pengine wao wenyewe watakuja ili waweze kubainishiwa. Hapo ndipo mwanafunzi atambainishia na Allaah amwongoze na kumlipa thawabu. Ama mijadala na mizozo mingi sio katika matendo ya Salaf. Matendo yao ilikuwa kubainisha na kusimamisha hoja kwa dalili za Qur-aan na Sunnah. Walikuwa wakitilia bidii kuzibainisha; yule mwenye kuzikubali ni sawa na yule asiyezikubali na akachagua kupotosha na kuwababaisha watu anaachwa, kukatwa na kutahadharishwa. Hivi ndivo walivokuwa wakifanya Salaf ili kuzuia madhara yake na kuepuka mitihani.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 82-83
  • Imechapishwa: 14/10/2019