Shirki ndogo. Ni yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah kwamba ni shirki, na kukathibiti dalili zengine ya kwamba mwenye shirki hiyo hatoki katika Uislamu. Imegawanyika katika aina mbili:

Aina ya kwanza: Ni shirki katika matamshi. Kama mtu kuapa kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah kakufuru au kashirikisha.”[1]

Vilevile kama mfano wa kusema:

“Lau kama si Allaah na wewe”

na

“Akitaka Allaah na wewe”.

Huku ni kushirikisha katika matamshi.

Aina ya pili: Shirki iliyojificha ndani ya nyoyo. Nayo ni aina mbalimbali. Kubwa katika hiyo ni riyaa. Kujionyesha kwa matendo. Nayo imegawanyika sampuli mbili:

1- Kujionyesha kwa wanafiki ambao wako katika tabaka la chini kabisa Motoni. Hawa wanajionyesha kwa watu kwa matendo yao na wala hawayaitakidi nyoyoni mwao. Bali ndani ya nyoyo zao mna kufuru. Huku ni kujionyesha ambako ni kufuru. Kwa sababu wenye nayo hawamuamini Allaah (´Azza wa Jall). Bali wajidhihirisha kwa matendo mema kwa ajili ya manufaa ya kidunia.

2- Kujionyesha ambako kunampitikia muislamu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia Maswahabah wake pindi ghafla alipojitokeza na akawakuta wanazungumzia ad-Dajjaal:

“Je, nisikwambieni kitu ambacho ninachokikhofia zaidi kwenu kuliko huyo al-Masiyh ad-Dajjaal?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah”. Akasema: “Ni kujionyesha. Anasimama mmoja wao na anaswali, akaipamba swalah yake kwa kuwa anaona watu wanamtazama.”[2]

Hii inaweza kunamtokea muislamu muumini na muumini ambapo akaingiwa ndani ya nafsi yake na kitu katika kujionyesha. Muislamu akiingiwa ndani ya nafsi yake na kitu katika kujionyesha, basi anatakiwa kupambana nacho na arudi kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Akipambana nayo haitomdhuru,. Ama akiendelea kuwa nayo, basi inabatilisha kile kitendo ikiwa kujionyesha huko alikuwa nako tokea mwanzo. Vilevile ikimtokea katikati ya kitendo na ikaendelea kwa mujibu wa maoni yaliyo na nguvu.

Kadhalika katika shirki iliyojificha ni kule mtu kutaka kusikika na kusifiwa. Ni jambo linatokea katika maneno yaliyowekwa katika Shari´ah kama vile kisomo, Adhkaar, kisomo na mengineyo anayoyafanya kwa sababu anataka watu wamsifu pale wanapomsikia au akaingiwa ndani ya nafsi yake na kitu katika kupenda sifa. Hii ni shirki ndogo.

Vivyo hivyo miongoni mwa shirki iliyojificha ni kule mtu kukusudia kwa matendo yake duniani. Akafanya matendo mema naye huku anataka mambo ya kidunia. Amesema (Ta´ala):

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ

“Yule anayetaka maisha ya dunia na mapambo yake, basi Tutawalipa kikamilifu matendo yao humo nao hawatopunjwa humo – hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote katika Aakhirah isipokuwa Moto.”

Yule mwenye kufanya matendo ya ´ibaadah mbalimbali na huku anataka manufaa ya kidunia, kama kwa mfano wale wanaotafuta elimu ya dini kwa ajili ya kutafuta dunia. Ama yule anayetafuta elimu isiyokuwa ya dini hakuna ubaya mtu akajifunza nayo kwa ajili ya manufaa ya kidunia. Mfano wa elimu hizo ni kujifunza hesabu, uhandisi na uandishi. Lengo lake kujifunza nazo ni kutaka apate kazi. Hizi hakuna ubaya wowote. Hizi ni miongoni mwa sababu zilizoruhusiwa na sio ´ibaadah. Ama kuhusu mambo ya ´ibaadah kama kw mfano mtu anaswali kwa ajili ya kutafuta dunia, anapambana Jihaad kwa ajili kutafuta kidunia, anajifunza elimu kwa ajili ya kutafuta dunia au anahiji kwa ajili ya kutafuta dunia, yote haya yanaingia katika Aayah hii:

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ

”Anayetaka maisha ya dunia na mapambo yake Tutawalipa kikamilifu ‘amali zao humo, nao hawatopunjwa humo. Hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote katika Aakhirah isipokuwa Moto.” (Hud 16:15)

“Ameangamia mja wa Khamiyswah, ameangamia mja wa Khamiylah, ameangamia mja wa Diynaar na Dirham. Akipewa anafurahi na asipopewa anakasirika.”[3]Mtu huyu ana matishio makali sana. Ni aina moja wapo ya shirki. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Hii ni aina ya shirki.

Mtu anatakiwa kumtakasia matendo yake Allaah (´Azza wa Jall). Akijiwa na kitu katika dunia bila ya kukikusudia, basi hiyo ni riziki aliyompa Allaah. Ama kufanya matendo ya Aakhirah kwa ajili ya dunia, hili ndilo lenye kusemwa vibaya na haya ndio yaliyotishiwa. Ni lazima kwa muislamu ayatakase matendo na maneno yake kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall).

[1] Ameipokea Ahmad (4904), at-Tirmidhiy (1535) na Abu Daawuud (3251). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri.”

Ameipokea vilevile al-Haakim (01/18) na (04/297) ambaye pia ameisahihisha kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] Ameipokea Ahmad (11252), Ibn Maajah (4204) na al-Haakim (04/329). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim na ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[3]Ameipokea al-Bukhaariy (2886).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 47-49
  • Imechapishwa: 13/07/2018