26. Mke anatakiwa kuhifadhi mali ya mume wake


Miongoni mwa haki za mume juu ya mke wake ni yeye kuihifadhi mali yake na asitumie chochote katika mali hiyo isipokuwa kwa idhini yake. Tumesikia jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyosema kuhusu wanawake bora:

“Ni yule anayemtii mume wake pindi anapomuamrisha, kumfurahisha pindi anapomtazama na kumhifadhi juu ya nafsi yake na mali yake.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si halali kwa mwanamke kutoa chochote katika mali ya mume wake isipokuwa kwa idhini yake.”[1]

Akimpa idhini ya kutumia na akatumia pasina uharibifu basi wote ni wenye kupewa ujira. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akitoa chakula kutoka kwenye nyumba yake pasina uharibifu anapata ujira wake kwa kile alichokitoa na mume wake kwa alichokichuma.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akitoa Swadaqah kutoka kwenye nyumba ya mume wake basi ana ujira na kadhalika mume wake anapata mfano wa hivo pasina chochote kupungua kwa sababu ya ujira wa yule mwingine.”[3]

Wanachuoni wamesema kuwa mwanamke anaweza kutoa kutoka kwenye nyumba ya mume wake, au mali ya mume wake, kwa njia tatu:

1- Mwanaume akampa idhini mke wake ya kutoa kwa njia maalum. Katika hali hii wote wawili wanalipwa ujira kikamilifu pasina ujira wa yeyote kupungua.

2- Mwanaume akampa mke wake idhini ya jumla ya kutoa katika mali yake. Katika hali hii wanalipwa ujira wote.

3- Mwanaume asimpe idhini mke wake ya kutoa katika mali yake. Katika hali hii lau [mwanamke] atatoa kitu katika mali yake [mume] atalipwa ujira na yeye [mwanamke] atapata madhambi.

[1] at-Twayaalisiy (1223) na kupitia mnyororo wa al-Bayhaqiy (4/8108). Imepokelewa vilevile na Ahmad (5/267), Abu Daawuud (3565), at-Tirmidhiy (670) na Ibn Maajah (2295) kwa muundo huu:

“Mwanamke asitumii chochote kutoka katika nyumba ya mume wake isipokuwa kwa idhini yake.”

Mnyororo wake ni mzuri – Allaah Akitaka. Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Targhiyb” (943).

[2] al-Bukhaariy (2065) na Muslim (1024). Muundo ni wa al-Bukhaariy.

[3] Ahmad (6/99), an-Nasaaiy (2539) na at-Tirmidhiy (671) ameifanya kuwa nzuri.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 24/03/2017