26. Malazimisho batilifu ya wakanushaji

´Aqiydah ya wakanushaji inapelekea katika malazimisho mengi batilifu. Baadhi yake ni yafuatayo:

1- Qur-aan na Sunnah imetamka waziwazi kwa ukafiri na kulingania katika ukafiri. Qur-aan na Sunnah vyote viwili ndani yake kumejaa sifa za Allaah ambazo kwa mujibu wa wakanushaji kuzithibitisha kunapelekea katika kufananisha na kufuru.

2- Qur-aan na Sunanh havikubainisha haki. Haki kwa mujibu wa watu hawa inapatikana kwa kukanusha sifa. Upande mwingine ni kwamba hamna ndani ya Qur-aan na Sunnah, si kwa waziwazi wala kwa dhahiri, lenye kuashiria kwamba sifa za Allaah zinatakiwa kukanushwa. Dalili kubwa zaidi ambayo bingwa wao anaweza kutumia ni kwa mfano maneno Yake (Ta´ala):

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua mwenye jina kama Lake?”[1]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

 “Na wala hana yeyote anayefanana [na kulingana] Naye.”[2]

Kila mwenye busara anajua kuwa Aayah hizi na mfano wake makusudio yake ni kumthibitishia Allaah (Ta´ala) ukamilifu na kwamba hakuna awezaye kuwa na sifa kama Zake. Haziwezi kuwa na maana kwamba hana sifa. Kwa hali hii ina maana kwamba Allaah ni mwenye kubabaisha katika maneno Yake au kwamba anatatiza au kwamba hawezi kuzungumza kwa ubainifu. Yote haya hayawezekani inapokuja katika maneno ya Allaah (Ta´ala) na maneno ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maneno ya Allaah na Mtume Wake wote wawili ndani yake mna ubainifu kamilifu na utashi kamilifu. Maneno haya hayana makusudio ya kuwapotosha viumbe na kuwapaka mchanga wa machoni. Maneno haya hayana kasoro katika ubainifu na ufaswaha.

3- Watu wa awali waliotangulia kati ya Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema ima walikuwa na ´Aqiydah batili na kuficha haki au walikuwa ni wajinga. Imepokelewa kwa mapokezi tele ya kwamba wanamthibitishia Allaah sifa kamilifu, ambazo watu hawa wanadai kwamba ni kosa. Hawakupatapo hata mara moja kukanusha kitu katika sifa za Allaah, jambo ambalo watu hawa ndilo wanalodai kuwa ni sawa. Ni jambo lisilowezekana kwa karne bora kuamini kitu kama hicho.

4- Allaah asingelisifika na sifa kamilifu, basi hilo linalazimisha asifiwe na sifa zenye mapungufu. Kila kinachopatikana basi ni lazima kiwe na sifa. Hivyo ikiwa Hasifiwi na sifa kamilifu, basi ni lazima awe ni mwenye kusifiwa na sifa zenye mapungufu. Hapa wakanushaji hawa wanaingia katika athari ya kujigonga na wanatumbukia katika kitu ambacho ni kibaya zaidi kuliko kile walichokikimbia.

[1] 19:65

[2] 112:04

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 11/05/2020