26. Kuhusu makuhani na mfano wao

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” kutoka kwa baadhi ya wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayemwendea mpiga ramli, akamuuliza juu ya kitu na akamsadikisha, basi hazitokubaliwa swalah zake kwa siku arubaini.”[1]

2- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayemwendea kunahi na akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Ameipokea Abu Daawuud.

3- Maimamu wane na al-Haakim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Atakayemwendea kunahi na akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[3]

al-Haakim amesema:

“Hadiyth ni Swahiyh kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

4- Abu Ya´laa amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri ya kwamba Ibn Mas´uud vilevile amesema hivo.

5- ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi yule atakayetafuta au akaomba kubashiriwa mikosi ya ndege, akafanya ukuhani au akafanyiwa ukuhani, akafanya uchawi au akafanyiwa uchawi. Atakayemwendea kuhani na akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea al-Bazzaar kwa cheni ya wapokezi nzuri na at-Twabaraaniy amepokea katika “al-Awsatw” kwa cheni ya wapokezi nzuri kupitia kwa Ibn ´Abbaas bila ya ziada ya neno:

“Na atakayemwendea kuhani… “

6- al-Baghawiy amesema: “Mpiga ramli ni yule anayedai kuvijua vitu vilivyoibiwa na vitu vilivyopotea na kama hayo kwa vitangulizi. Imesemekana vilevile kwamba ni kuhani. Kuhani ni yule anayeelezea juu ya vitu vilivyofichikana katika mustakabli. Imesemekana vilevile kwamba ni yule anayeelezea juu ya vitu vilivyomo katika dhamira ya mtu.”

7- Abul-´Abbaas bin Taymiyyah amesema:

“Mpiga ramli ni jina la kuhani, mtabiri wa nyota, mwaguzi na mfano wao katika wanaoongelea kuyajua mambo kwa kutumia njia hizi.”

8- Ibn ´Abbaas amesema kuhusu watu wanaoandika “Abaa Jaad” na wanatazama nyota:

“Sioni wanaofanya hivyo kuwa wana sehemu yoyote mbele ya Allaah.”

MAELEZO

Mlango unaowazungumzia wapiga ramli, waguzi na wengineo wanaodai kuyajua mambo yaliyofichikana.

Makuhani ni wale wanaoshirikiana na majini. Watu kama hawa wanatakiwa kutokomezwa, kuwaaziri, kuwakadhibisha na kutowauliza kitu.

1- Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” kutoka kwa baadhi ya wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayemwendea mpiga ramli, akamuuliza juu ya kitu na akamsadikisha, basi hazitokubaliwa swalah zake kwa siku arubaini.”

Wanachuoni wanasema kuwa wakeze ni Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

Sentesi “na akamsadikisha” haiko katika Muslim. Ima mwandishi ameteleza au amenukuu kutoka katika nusukha ambayo iko na maneno haya. Sentesi “na akamsadikisha” iko kwa Ahmad.

Upokezi kwa Muslim unathibitisha kuwa kule kuwauliza tu haijuzu kwa sababu kunawakweza wapiga ramli na kunapelekea uchawi wao kusadikishwa na kuadhimishwa huko mbeleni. Kwa ajili hiyo inapaswa kuachana nao na kuwapuuza. Muslim amepokea kupitia kwa Mu´aawiyah bin al-Hakam ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wao si lolote si chochote. Usiwaendee.”

Hivi ndivo wanavotakiwa kutaamiliwa ili wao na mfano wao watwezwe, wapuuzwe na kutokomezwa.

2- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayemwendea kunahi na akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea Abu Daawuud.

3- Maimamu wane na al-Haakim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Atakayemwendea kunahi na akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi amekufuru yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Hadiyth inafahamisha kwamba kuwaendea haijuzu na kuwasadikisha katika mambo yanayohusiana na kudai mambo yaliyofichikana ni kufuru. Kwa sababu hakuna ajuaye mambo yaliyofichikana isipokuwa Allaah pekee. Watu hawa sio Mitume. Kuhani ni kafiri akisema kuwa yeye anajua mambo yaliyofichikana. Mwenye kumsadikisha pia kwamba anajua mambo yaliyofichikana ni kafiri kwa sababu hakuamini maneno Yake (Ta´ala):

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ

“Sema: “Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye yaliyofichikana isipokuwa Allaah.” (an-Naml 27:65)

Kwa ajili hiyo ni wajibu kutahadhari nao.

4- Abu Ya´laa amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri ya kwamba Ibn Mas´uud vilevile amesema hivo.

5- ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi yule atakayetafuta au akaomba kubashiriwa mikosi ya ndege, akafanya ukuhani au akafanyiwa ukuhani, akafanya uchawi au akafanyiwa uchawi. Atakayemwendea kuhani na akamsadikisha kwa aliyoyasema, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea al-Bazzaar kwa cheni ya wapokezi nzuri na at-Twabaraaniy amepokea katika “al-Awsatw” kwa cheni ya wapokezi nzuri kupitia kwa Ibn ´Abbaas bila ya ziada ya neno:

“Na atakayemwendea kuhani… “

Haya ni makemeo na ni matishio kwa yule anayefanya mambo kama haya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… si katika sisi.”

Bi maana si katika wale wanaofuata Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama kuhusu Takfiyr, japokuwa udhahiri wake unafahamisha Takfiyr, inachukuliwa kutoka katika dalili zengine zilizopambanua suala hili. Haijalishi kitu mtu ameamini mkosi wa ndege juu ya nafsi yake mwenyewe au amewaomba wengine wambashirie mkosi wa ndege, amejifanyia ukuhani mwenyewe au amewaomba wengine wamfanyie ukuhani kwa kuridhia kwake. Kuhusu Takfiyr inatakiwa kupambanuliwa kama tulivyotangulia kusema. Kuwasadikisha ni kufuru kubwa. Mwenye kudai kujua mambo yaliyofichikana basi anatakiwa kuambiwa kutubia. Ima atubie au auawe. Ikiwa atasema kuwa hajui mambo yaliyofichikana, basi atatakiwa kuaziriwa ili asije kurudi tena katika mambo hayo.

6- al-Baghawiy amesema: “Mpiga ramli ni yule anayedai kuvijua vitu vilivyoibiwa na vitu vilivyopotea na kama hayo kwa vitangulizi. Imesemekana vilevile kwamba ni kuhani. Kuhani ni yule anayeelezea juu ya vitu vilivyofichikana katika mustakabli. Imesemekana vilevile kwamba ni yule anayeelezea juu ya vitu vilivyomo katika dhamira ya mtu.”

Vitangulizi inahusiana na vitu anavyopanga na baadaye vinamjulisha mahali kulipoibiwa kitu fulani. Kwa mfano anaweza kujua kwa nyayo za mnyama na nyasi zake. Haya ni mambo yanaweza kutokea, lakini mpiga ramli anakuwa ni mwenye kusemwa vibaya pindi anapodai kutambua mambo yaliyofichikamana. Ama kuhusu mambo yenye kuhisiwa hayaingii katika mlango huu.

Mpiga ramli anasema vile vilivyomo katika dhamira ya mtu. Hayafikii hayo isipokuwa kwa kuwauliza mashaytwaan na majini.

Faida

Haijuzu kujifunza uchawi kwa hali yoyote ile hata kama lengo la mtu ni kutaka kuzingua uchawi. Kwa sababu mtu hawezi kulifikia hilo isipokuwa kwa kumuabudu asiyekuwa Allaah, kufanya yale aliyoharamisha Allaah au kuacha yale Allaah aliyowajibisha.

7- Abul-´Abbaas bin Taymiyyah amesema:

“Mpiga ramli ni jina la kuhani, mtabiri wa nyota, mwaguzi na mfano wao katika wanaoongelea kuyajua mambo kwa kutumia njia hizi.”

Maandiko yote haya yanafahamisha ya kwamba kuhani, mchawi, mtabiri wa nyota, mwaguzi na mfano wao ni wenye kusemwa vibaya na kwamba wanadai kuyajua mambo yaliyofichikana.

8- Ibn ´Abbaas amesema kuhusu watu wanaoandika “Abaa Jaad” na wanatazama nyota:

“Sioni wanaofanya hivyo kuwa wana sehemu yoyote mbele ya Allaah.”

Bi maana zile herufi za alfabeti a, b, j, d. Wanaziandika herufi hizo, wanaziweka baadhi juu ya zengine na wanasema kwamba kutatokea kitu fulani na fulani. Kusema kwamba hawana sehemu yoyote mbele ya Allaah ni kwamba hawana fungu lolote kwa sababu ni wenye kudai kuyajua mambo yaliyofichikana.

[1] Muslim (2230).

[2] Abu Daawuud (3904), Ibn Maajah (639) na ad-Daarimiy (1136). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (3387).

[3] Ahmad (9532), al-Hakim (15) na al-Bayhaqiy (16273). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (5939).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 94-96
  • Imechapishwa: 16/10/2018