Miongoni mwa wanawake wa Kiislamu wako ambao  wanafanya unafiki katika Hijaab. Wanapokuwa katika jamii inayovaa Hijaab nao wanavaa Hijaab. Na wanapokuwa katika jamii isiyovaa Hijaab nao hawavai Hijaab. Miongoni mwao wako ambao wanavaa Hijaab wanapokuwa sehemu ya ummah na wanapoingia sehemu ya biashara, hospitali, anamzungumzisha mmoja katika masonara au mmoja wapo katika mafundi wa nguo za wanawake, basi anafunua uso wake na mikono yake kana kwamba yuko mbele ya mume wake au mmoja katika Mahram zake. Mcheni Allaah enyi mnaofanya mambo hayo.

Tumewashuhudia baadhi ya wanawake wanaofika kwenye uwanja wa ndege wanaotoka nje ya nchi ambao hawavai Hijaab isipokuwa pale ambapo ndege inadema katika moja ya viwanja vya ndege vya nchi hii. Ni kama kwamba Hijaab imekuwa ni katika desturi na sio katika mambo yaliyowekewa Shari´ah na dini hii.

Ee dada wa Kiislamu! Hakika Hijaab inakulinda na inakuhifadhi kutokamana na macho yenye sumu yanayotoka kwa wale ambao mioyoni mwao mna maradhi na mijibwawatu na isitoshe inakata zile tamaa zao. Hivyo basi, lazimiana nayo na shikamana nayo barabara. Usijali propaganda zenye kubabaisha zinazoipiga vita Hijaab na kuidogesha. Kwani hakika si vyengine wanakutakia shari. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَن تَمِيلُوا مَيْلًا عَظِيمًا

“Wale wanaofuata matamanio wanataka mkengeuke, mkengeuko mkubwa mno.”[1]

[1] 04:27

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 52
  • Imechapishwa: 31/10/2019