26. Dalili kwamba Allaah haridhii kushirikishwa na yeyote

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

MAELEZO

Allaah hayuko radhi kushirikishwa na yeyote awaye, jambo ambalo liko wazi ndani ya Qur-aan na Sunnah. Lakini hili ni kwa yule anayeelewa, akazingatia, akatupilia mbali mambo ya kufuata kichwa mchunga, sababu batili na akazinduka kwa nafsi yake. Dalili juu ya kwamba Allaah haridhii kushirikishwa pamoja Naye mwengine yeyote awaye ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”

Misikiti ni zile nyumba za Allaah na ni sehemu zilizotengwa kwa ajili ya kuswalia. Ndio maeneo yanayopendwa zaidi na Allaah, ndio nyumba ambazo Allaah ameidhinisha zitukuzwe na litajwe ndanbi yake jina Lake. Ni lazima misikiti hii iwe ni sehemu za kumwabudu Allaah pekee. Kusizushwe ndani yake kitu kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah. Kwa msemo mwingine kusijengwe ndani yake makaburi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwenye kufanya hivo na akaeleza kuwa hicho ndicho kitendo cha mayahudi na manaswara na akatukataza jambo hilo mwishoni mwa uhai wake alipokuwa anataka kukata roho (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kusema:

“Zindukeni! Hakika waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi kuwa ni misikiti.”[2]

Aliyasema maneno haya kipindi alipokuwa anataka kukata roho:

“Zindukeni! Msilifanye kaburi langu kuwa sehemu ya kuswalia. Kwani hakika mimi nakukatazeni jambo hilo.”

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu ya kuswalia.”[3]

Ni lazima misikiti kuitakasa kutokamana na athari ya shirki na mizimu. Kusijwengwe juu ya makaburi au wakazikwa ndani yake wafu baada ya kujengwa kwake. Bali misikiti inapaswa iwe ni mahali pa kumwabudu Allaah peke yake. Kusimamishwe ndani yake swalah, kutajwa ndani yake jina la Allaah, kusomwe ndani yake Qur-aan, kufanywe ndani yake darsa zenye manufaa na watu wabaki ndani yake kwa muda mrefu kwa ajili ya ´ibaadah. Hizi ndio kazi za misikiti. Ama kuwekwa ndani yake masanamu yanayoabudiwa badala ya Allaah, basi hiyo itakuwa sio misikiti. Bali itakuwa ni mashaahid za shirki licha ya kuwa watetezi wayo wataita kuwa ni misikiti:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah.”

Bi maana si ya mwengine. Jengine ni kwa sababu misikiti ndio sehemu zinazowakusanya watu na wakakutana. Kwa hiyo ni lazima kuisafisha kutokamana na shirki, Bid´ah na mambo ya ukhurafi. Watu wanapokea ndani yake elimu na ´ibaadah. Kwa hiyo kukipatikana ndani yake kitu katika shirki na mambo ya ukhurafi wataathirika kwayo na kuyaeneza ardhini. Kwa hiyo ni lazima misikiti itakaswe kutokamana na shirki. Mkubwa kuliko yote ni msikiti Mtakatifu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameamrisha kuusafisha. Amesema (Ta´ala):

وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ

“Tulipomweka Ibraahiym mahali pa nyumba Tukamwambia: “Usinishirikishe na chochote na isafishe nyumba Yangu kwa wafanyao Twawaaf na wanaosimama kuswali na wanaorukuu na kusujudu.”[4]

Kuitakasa kutokamana na nini? Kuitakasa kutokamana na shirki, Bid´ah na mambo ya ukhurafi. Vilevile inatakiwa kuisafisha kutokamana na uchafu na taka.

Maneno Yake (Ta´ala):

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe [msimuabudu] yeyote pamoja na Allaah.”

Enyi watu! Msiombe yeyote pamoja na Allaah. Msimtake msaada yeyote pamoja na Allaah. Kwa mfano mtu akasema “Ee Allaah! Ee Muhammad! Ee ´Abdul-Qaadir!” au mtu akasema “Ee ´Abdul-Qaadir! Ee Muhammad! na mfano wa hayo. Allaah hayuko radhi na hilo na wala hayakubali. Maneno Yake:

أَحَدًا

“… yeyote.”

Ukanushaji uliokuja katika mazingira ya kukanusha na hivyo unamkusanya kila mmoja. Hakubaguliwi yeyote; si Malaika aliyekaribu, wala Mtume aliyetumwa, wala sanamu, wala mzimu, wala Shaykh, wala walii, wala aliyehai, wala aliyekufa. Haijalishi kitu ni nani. Makatazo hayo yamemkusanya kila mwenye kuombwa badala ya Allaah:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe [msimuabudu] yeyote pamoja na Allaah.”

Aayah hii imefahamisha kuwa ´ibaadah haisaidii kitu isipokuwa pamoja na Tawhiyd na kwamba inabatilika pale inapokuwa imechanganyikana na shirki na inakuwa ni janga kwa mwenye nayo. Jengine ni kwamba maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah.”

yanaonyesha kwamba ni lazima mtu ajenge jengo kwa ajili ya Allaah. Makusudio ya kujenga isiwe kujionyesha, kutaka kusikika au makumbusho, kama wanavosema, na kuwepo na athari za Kiislamu. Yote haya ni batili. Misikiti inajengwa kwa ajili ya ´ibaadah na kwa malengo ya ´ibaadah na nia mtu amkusudie Allaah (´Azza wa Jall).

Jengine ni kwamba misikiti inatakiwa kujengwa kwa chumo zuri. Haitakiwi kujengwa kwa chumo la haramu. Kwa sababu Allaah ni ya Allaah (´Azza wa Jall):

“Na Allaah hakubali isipokuwa kilicho kizuri.”

Kwa hiyo kujenga msikiti kutokane na matumizi ya halali. Nia ya mjengaji iwe imetakasika kwa ajili ya uso wa Allaah  (´Azza wa Jall). Hakusudii kwa kujenga masifa kutoka kwa watu, kubaki ukumbusho wake, kujionyesha au kutaka kusikika. Kujenga misikiti ni ´ibaadah na ´ibaadah ni lazima iwe takasifu kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall).

[1] 72:18

[2] Muslim (532).

[3] al-Bukhaariy (435, 436) na Muslim (531).

[4] 22:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 56-60
  • Imechapishwa: 03/12/2020