25. Tafsiri ya Hadiyth ya al-Fadhwl

3- Hadiyth ya Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) haitolea dalili yoyote ya kujuzusha kumtazama mwanamke ajinabi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuitikia al-Fadhwl kwa kitendo chake; bali aligeuza uso wake upande mwingine. Ndio maana an-Nawawiy ametaja katika tafsiri yake “as-Swahiyh” ya Muslim kwamba Hadiyth inatolea dalili juu ya uharamu wa kumwangalia mwanamke ajinabi. Haafidhw Ibn Hajar amesema katika “Fath-ul-Baariy” ya kwamba Hadiyth inatolea dalili juu ya uharamu wa kumwangalia mwanamke ajinabi na kuwa ni wajibu kushusha macho. ´Iyaadhw amesema kuwa baadhi ya wanachuoni wanasema sio wajibu ikiwa hakukhofiwi fitina lakini kitendo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa al-Fadhwl kinasema mengi kuliko maneno.

Lau mtu atauliza ni kwa nini basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuamrisha mwanamke kufunika uso, udhahiri ni kwamba alikuwa katika Ihraam. Katika hali hii ni jambo ambalo halikuwekwa kwenye Shari´ah kwake kufunika uso ikiwa kama hachelei kuna ajinabi yeyote anayemwona. Kuna uwezekano vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia baada ya hapo. Kwa sababu tu haikupokelewa haina maana kwamba haikutendeka. Kwa sababu kukosekana mapokezi hakuna maana yanakosekana mapokezi. Muslim na Abu Daawuud wamepokea kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya mtazamo wa ghafla ambapo akasema: “Tazama kando.” Au akaniamrisha nitazame kando.”[1]

[1] Muslim (2159) na Abu Daawuud (2148).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 26/03/2017