Suala la tatu: Yaliyochukizwa na kuharamishwa wakati wa funga

1- Imechukiza kuupwekesha mwezi wa Rajab kwa funga. Kwa sababu kufanya hivo ni katika kujifananisha na watu wa kipindi cha kikafiri. Walikuwa wakiutukuza mwezi huu. Endapo mtu ataufunga pamoja na kuambatanisha na mwezi mwingine haitokuwa imechukizwa. Katika hali hiyo atakuwa si mwenye kuupwekesha kwa funga. Ahmad bin Khurshah bin al-Harr amesema:

“Nilimuona ´Umar bin al-Khattwaab akiwapiga wenye kufunga katika Rajab ili waiweke mikono yao kwenye chakula na akisema: “Kuleni! Ni mwezi ambao ulikuwa ukiadhimishwa na watu wa kipindi cha kikafiri.”[1]

2- Imechukizwa kupwekesha siku ya ijumaa kwa kufunga. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msifunge siku ya ijumaa; isipokuwa kwa kufunga siku moja kabla yake au baada yake.”[2]

Hakuna neno endapo ataifunga pamoja na siku nyingine. Hilo ni kutokana na Hadiyth iliotangulia.

3- Imechukizwa kupwekesha siku ya jumamosi kwa funga. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msifunge siku ya jumamosi isipokuwa kwa yale mliyofaradhishiwa.”[3]

Kinacholengwa ni kuifunga yenyewe peke yake na kukusudia kufunga siku hiyo. Lakini endapo mtu atafunga na siku nyingine tena hakuna neno. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akimwambia mama wa waumini Juwayriyah alikuwa ameingia nyumbani kwake siku ya ijumaa akamkuta amefunga: “Jana ulifunga?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Umekusudia kufunga kesho?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Basi fungua.”[4]

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Umekusudia kufunga kesho?”

juu ya kwamba inafaa kufunga jumamosi pamoja na siku nyingine.

Imaam at-Tirmidhiy (Rahimahu Allaah) amesema punde tu baada ya kutaja Hadiyth iliyokwishatangulia:

“Maana ya machukizo ni mtu akapwekesha kufunga siku ya jumamosi peke yake. Kwa sababu mayahudi wanaitukuza jumamosi.”

[1] al-Albaaniy ameiegemeza kwa Ibn Shaybah kisha akasema: ”Swahiyh”. Tazama ”Irwaa´-ul-Ghaliyl” (04/113).

[2] al-Bukhaariy (1985) na Muslim (1144).

[3] Abu Daawuud (2421), at-Tirmidhiy (744), Ibn Maajah (1726) na al-Haakim (01/435). Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na al-Haakim ameifanya kuwa ni nzuri kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy ambapo adh-Dhahabiy akaafikiana naye. al-Albaaniy pia ameisahihisha katika “Swahiyh-ut-Tirmidhiy” (594).

[4] al-Bukhaariy (1986).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 164-165
  • Imechapishwa: 16/05/2020