25. Radd juu ya utata wa visa vya uongo na ndoto zinazopingana na Shari´ah

Kumi: Kutegemea kwao simulizi na visa ya kwamba kuna mtu fulani ambaye aliliendea kaburi fulani ambapo akapata kitu kadhaa na kwamba kuna mtu fulani ameona ndotoni kitu kadhaa na kadhaa. Mfano wa visa hivyo ni kile kinachosimuliwa na baadhi yao kwamba al-´Utaybiy ameeleza:

“Nilikuwa nimeketi kwenye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo nikamuona mbedui anakuja na kusema: “Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Mtume wa Allaah. Nimemsikia Allaah akisema:

وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا

“Lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia wakamuomba Allaah msamaha na Mtume akawaombea msamaha, basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.”[1]

Nimekuja hali ya kusamehewa madhambi yangu na hali ya kukuomba uombezi kwa Mola wangu. Kisha yule mbedui akaondoka zake. Baadaye nikamuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndotoni akisema:

“Ee al-´Utaybiy! Ni haki kwa huyo mbedui. Mbashirie kwamba Allaah amemsamahe.”

Jibu ni kwamba visa na ndoto si dalili yenye kusilihi kujenga juu yake hukumu na mambo ya ´Aqiydah. Ama kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

جَاءُوكَ

“… wangelikujia… “

kinachokusidiwa ni kwenda kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati bado yuiko hai. Hakumaanishwi kuliendea kaburi lake. Dalili ya hilo ni kwamba hakuna Swahabah wala wale waliowafuata kwa wema hata mmoja ambaye alikuwa akienda kwenye kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuomba amuombee msamaha pamoja na kwamba walikuwa na pupa kubwa juu ya kheri na kutekeleza amri. Lau hilo lingekuwa ni jambo linalokubalika Kishari´ah basi wangelitekeleza.

[1] 04:64

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 02/04/2019