1- Anayeweza kumsaidia nduguye kwa kitu kitachosahilisha msiba au tatizo lake asiache kufanya hivo.

2- Aliye na busara hatakiwi kufunga udugu na mtenda dhambi. Mtenda dhambi ni kama nyoka kiziwi ambaye hawezi jengine isipokuwa kuuma na kutia sumu. Mtenda dhambi hana mawasiliano na wala hajengi udugu isipokuwa tu kwa ajili ya kutaka kujinufaisha mwenyewe. Mtukufu anampenda mtukufu tangu pale mara ya kwanza wanakutana, hata kama hawakutani mara nyingi.

3- Sufyaan ameeleza kuwa Yuunus bin ´Ubayd alipatwa na msiba. Kukasemwa: “Ibn ´Awf si alikutembelea?” Akasema: “Tukiamini mapenzi ya ndugu zetu hatudhuriki kwa yeye kutotutembelea.”

4- Mwenye busara anatakiwa kuhakikisha asiwe ni mkosefu wa adabu kwa nduguze. Akitumbukia kwenye kitu kama hicho ahakikishe amekisitisha mara moja. Asichukulie jepesi jambo la ukosefu wa adabu. Mwenye kupuuzia dogo anaweza kutumbukia katika kubwa. Anatakiwa kuhakikisha amesitisha mara moja. Hakuna kheri katika ukweli pasi na kutekeleza na hakuna kheri katika elimu pasi na uchaji.

5- Aliye na busara haungi udugu isipokuwa na watu wenye fikiria vyema, watu wenye dini, elimu, tabia njema, wenye akili na wamekulia na watu wema. Kutangana na mpumbavu aliyekulia na watu wema ni bora kuliko kutangamana na mwerevu aliyekulia na watu wajinga.

6- Mwenye busara huwachunguza ndugu zake kabla ya kuunga nao udugu. Moja katika uzoefu bora kabisa ni mtu kuwa na mapenzi tele sawa na anapokuwa amekasirika.

7- Luqmaan amesema:

“Ee mwanangu! Unapotaka kuunga udugu na mtu basi anza kwanza kumkasirisha. Asipokuwa na uadilifu kwako pindi amekasirika basi achana naye.”

8- Shu´bah amesema:

“Ibn Mas´uud aliwatokea marafiki zake akawaambia: “Nyinyi mnaondoa huzuni wangu.”

9- Khaalid bin Swafwaan amesema:

“Hakukubaki ladha katika dunia hii isipokuwa mambo matatu; kukaa na wanawake, kuwanusa watoto na kukutana na ndugu.”

10- Mwenye busara anatakiwa kutambua kuwa hakuna furaha inayoweza kulinganishwa na kutangamana na ndugu na hakuna hamu inayoweza kulinganishwa kama kuwakosa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 88-93
  • Imechapishwa: 14/02/2018