25. Msimamo wa madhehebu mbalimbali juu ya Maswahabah

Wale waliopotea katika haya wamegawanyika mapote mawili:

1-  Nawaaswib.

2- Khawaarij.

Raafidhwah wanawakufurisha Maswahabah na hawabagui isipokuwa Maswahabah wanne tu; ´Aliy, Abu Dharr, Salmaan na Miqdaad bin al-Aswad. Wanachupa mpaka juu ya ´Aliy na wanasema kuwa ´Aliy ndiye wasii baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba uongozi wa Abu Bakr ni dhuluma na uporaji na kwamba uongozi wa ´Umar na ´Uthmaan yote hayo ni dhuluma na uporaji. Kwa sababu wanaona kuwa uongozi ni wa ´Aliy.

Kuhusu Nawaaswib wanamchukia ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na wanamtukana yeye na kizazi chake.

Khawaarij wamewakufurisha Maswahabah wote.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanawapenda Maswahabah wote wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakiwemo watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo. Wanawapenda wote na hawatenganishi kati yao. Ni kweli kwamba baadhi ni wabora kuliko wengine. Makhaliyfah waongofu na wale wengine waliobaki katika wale kumi waliobashiriwa Pepo ni wabora kuliko Maswahabah wengine. Waliopigana vita vya Badr ni wabora kuliko wengine. Waliokula kiapo chini ya mti na Muhaajiruun ni wabora kuliko Answaar. Lakini ubora haupelekei kumtukana yule anayeshindwa ubora au kumsema kwa ubaya. Wote wana ubora wa uswahabah kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako kati na kati juu ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kati ya Raafidhwah, Khawaarij na Nawaaswib. Wanawapenda wote na wakiwemo watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanawaheshimu. Lakini hata hivyo hawachupi mpaka kwao kama wanavofanya Raafidhwah mpaka wakafikia kusema kwamba uongozi ni wa ´Aliy na kizazi chake na kwamba Maswahabah waliwapora na wakawadhulumu. Wanamlaani Abu Bakr na ´Umar na wanawaita kuwa ni masanamu ya Quraysh – Allaah awakabehi. Kila Aayah iliotaja dhuluma au kufuru wanaiteremsha kwa Maswahabah. Maneno yake:

“Wako kati na kati katika mlango wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kati ya Raafidhwah na Khawaarij.”

baina ya Raafidhwah na Khawaarij na Nawaaswib pia. Khawaarij wamemkufurisha ´Aliy na ´Uthmaan na wengi katika Maswahabah. Upande wa pili Raafidhwah wamefanya kinyume chake wamechupa mpaka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), wakaamini kuwa ndiye khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwamba ndiye wasii na kwamba Maswahabah ni madhalimu na kwamba wamempora haki yake.

Khawaarij wao wamemkufurisha ´Aliy na Maswahabah. Raafidhwah ni kinyume chao wamechupa mpaka kwa ´Aliy kiasi cha kwamba wale waliopindukia katika wao wanasema kuwa yeye ndiye Allaah. Wale ambao sio wapetukaji hawasemi kuwa yeye ni Allaah. Lakini hata hivyo wanawakufurisha Maswahabah, wanawasifia dhuluma na ukandamizaji, wanawalaani na kuwatukana. Wako pande mbili zinazogongana.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah – kama tulivyotangulia kusema – wanawapenda Maswahabah wote na wanatambua hadhi ya watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawakutenganisha baina ya yeyote katika wao kwa sababu ya kutendea kazi wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ndio madhehebu yao juu ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Wao ndio wabora wa Ummah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wabora wenu ni karne yangu, kisha wale wataofuatia, kisha wale wataofuatia.”[1]

Wao karne bora, wao ndio wabora wa Ummah, wao ndio ambao Allaah (Jalla wa ´Alaa) na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameusia juu yao.  Wao ndio ambao wameeneza Uislamu kutokana na yale waliyopokea kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakawafikishia Ummah. Hakuna njia nyingine umetufikia Uislamu huu tulonao isipokuwa kupitia kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Wao ndio kiunganishi chetu kati yetu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hadiyth zote wpokezi wake ni Maswahabah ambao wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa kifupi ni kwamba hii ndio ´Aqiydah ya Shaykh. Ni ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wale wanaosema kuwa Shaykh ni katika Khawaarij na kwamba anakufurisha watu wamemsemea uongo.

[1] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2535) kupitia kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 27/03/2021