Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaona kuwa Maswahabah bora ni wale wane. Mbora wao ni Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan halafu ´Aliy. Mpangilio wao katika fadhilah ni sawa na mpangilio wao katika uongozi. Lakini kitendo cha Abu Bakr kuwa ndiye mbora haina maana kwamba hakuna mmoja katika Maswahabah ambaye anaweza kuwa na sifa nzuri maalum akamshinda Abu Bakr. Kwa mfano ´Aliy bin Abiy Twaalib anaweza kuwa na sifa nzuri asiyokuwa nayo Abu Bakr. ´Umar anaweza kuwa na sifa nzuri asiyokuwa nayo Abu Bakr. Vivyo hivyo kwa ´Uthmaan.

Kuzungumzia fadhilah zilizoachiwa na ngazi za kijumla zilizoenea basi itambulike kuwa ngazi za Maswahabah zinatofautiana kwa maafikiano ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa mujibu wa dalili za Qur-aan na Sunnah. Khaalid bin al-Waliyd na ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf walizozana juu ya jambo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema kumwambia Khaalid:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake lau mmoja wenu atatoa dhahabu kiasi cha mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vilivyojazwa na mikono vya mmoja wao wala nusu yake.”[1]

[1] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (254).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 37
  • Imechapishwa: 20/08/2019