25. Kumthibitishia Allaah sifa ya mwanzo, ya mwisho, ya ujuzi na kulingana juu ya ´Arshi


Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

14- Mola wetu ni wa Mwanzo pasi na [kuuliza] ni lini [ameanza] na ni wa Mwisho pasi na kikomo. Anayajua ya siri na yaliyofichikana na amelingana juu ya ´Arshi. Elimu Yake iko kila mahali na haikosekani mahali kote.

MAELEZO

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ni wa mwanzo bila ya kuwa na mwisho na ni wa mwisho bila ya kuwa na ukomo. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ

“Yeye ndiye wa mwanzo na wa mwisho na Aliye juu na Aliye karibu.” (57:03)

Majina yanayokabiliana. Wa mwanzo linakabiliwa na wa mwisho, Aliye juu linakabiliwa na Aliye karibu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifasiri Aayah hii pale aliposema:

“Wewe ni wa mwanzo na hakuna kitu kabla Yako, Wewe ni wa mwisho na hakuna kitu baada Yako, Wewe ndiye Uliye juu na hakuna kitu juu Yako na Wewe ndiye Uliye karibu na hakuna kitu karibu kuliko Wewe.”[1]

Hii ndio tafsiri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anajitokeza mtu na kufasiri kinyume na tafsiri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema kwamba Aliye juu (adh-Dhwaahir) maana yake ni kwamba amedhihiri kwa akili na amedhihiri kwa hoja na kwamba haina maana kuwa yuko juu ya viumbe wote au kwamba amelingana juu ya ´Arshi. Hili ni batili. Hii sio tafsiri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kiumbe ambaye anamjua zaidi Allaah ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amefasiri Aayah hii kwa tafsiri ilio wazi na kusema kwamba wa mwanzo ni ambaye hakuna kabla Yake kitu. Kwa msemo mwingine ni wa kwanza asiyekuwa na mwanzo. Wa mwisho ni ambaye hakuna baada Yake kitu. Bi maana ni wa mwisho bila ya kuwa na kikomo. Aliye juu ni ambaye hakuna kitu juu yake. Bi maana Yuko juu ya viumbe:

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ

“Naye yu juu ya waja Wake.” (06:18)

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً

“Naye yu juu ya waja Wake na anakutumieni walinzi.” (06:61)

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye yu juu ya waja Wake, Naye ni Mwenye hekima, Mjuzi.” (06:18)

Yeye (Ta´ala) ana Ujuu wa Dhati, Ujuu wa hadhi na Ujuu wa  nafasi.

“Wewe ndiye Uliye karibu na hakuna kitu karibu kuliko Wewe.”

Bi maana anakijua kila kitu na hakifichikani Kwake kitu chochote. Pamoja na kwamba Yuko juu ya viumbe Vyake, hata hivyo hafichikani na kitu katika yaliyo ndani mwao na yaliyofichikana kwenye vifua vyao. Vilevile hafichikani na kitu ardhini wala mbinguni (Subhaanahu wa Ta´ala). Baada ya haya yote anajitokeza mtu na kusema kwamba Allaah (Jalla wa ´Alaa) hayuko juu, hayuko chini, hayuko kuliani wala kushotoni, hayuko ndani ya ulimwengu na wala nje ya ulimwengu. Hii ina maana kwamba hayupo sasa. Haya yanapatikana kwenye vitabu vya wanafalsafa.

[1] Muslim (2713).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 61
  • Imechapishwa: 08/01/2018