25. Hakuna mgongano kati ya aliyosimulia Ibn ´Abbaas na ´Aaishah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa pia kuamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake. Imepokelewa Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Qataadah amepokea hilo kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

al-Hakam bin Abaan amepokea hilo kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

´Aliy bin Zayd amepokea hilo kutoka kwa Yuusuf bin Mahraan, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

Tunaiamini Hadiyth hii kama ilivyo kama jinsi ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni uzushi kuzungumzia juu ya hilo. Tunaliamini kama lilivyo kama jinsi ilivyofikishwa na hatujadili na yeyote juu ya suala hili.

MAELEZO

Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´annumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake duniani. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amelipinga hilo na akasema kwamba madai hayo ni uongo mkubwa. Udhahiri ni kwamba maandiko hayo mawili yanagongana, lakini wanachuoni wameyaoanisha na wakasema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake duniani kwa moyo wake na sio kwa macho yake. Hivo ndivo walivyoaonisha uthibitishaji wa Ibn ´Abbaas na upingaji wa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhum). Hivyo mgongano unaondoka. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa kama amemuona Mola wake, akajibu:

“Ni nuru. Vipi nitamuona?”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 “Allaah halali na wala haimstahikii Yeye kulala. Anaishusha mizani na kuinyanyua. Kwake kunapandishwa matendo ya usiku kabla ya mchana na matendo ya mchana kabla ya usiku. Pazia Yake ni nuru; lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila anachoona katika uumbaji Wake.”[2]

[1] Muslim (178).

[2] Muslim (179).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 80
  • Imechapishwa: 14/10/2019