al-Hijaab maana yake ni kwamba mwanamke ajisitiri mwili wake wote mbele ya wanaume ambao sio katika Mahram zake. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ

“Wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, baba zao, baba za waume wao, wana wao wa kiume, wana wa kiume wa waume zao, kaka zao, wana wa kiume wa kaka zao, wana wa kiume wa dada zao… “[1]

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ

“Mnapowauliza haja, basi waulizeni nyuma ya pazia.”[2]

Makusudio ya Hijaab ni kile kinachomsitiri mwanamke katika ukuta, mlango au vazi. Tamko la Aayah, japokuwa ni lenye kuwazungumzisha wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi itambulike kuwa hukumu yake ni yenye kuenea kwa wanawake wote. Kwa sababu ametoa sababu kwa maneno Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”[3]

Sababu hii ni yenye kuenea. Ueneaji wa sababu yake ni dalili juu ya kuenea kwa hukumu yake. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake [wote] wa Waumini – ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie jilbaab zao.”[4]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“al-Jilaab ndio buibui na ndio ile ambayo Ibn Mas´uud na wengineo wanaita kuwa ni Ridaa´. Watu wa kawaida wanaita kuwa ni Izaar. Nayo ni ile Izaar kubwa inayofunika kichwa chake na mwili wake wote. Abu ´Ubaydah na wengineo wamesimulia kwamba inateremshwa kuanzia juu ya kichwa chake na kusionekane isipokuwa macho yake. Miongoni mwa aina zake pia ni Niqaab.”[5]

Miongoni mwa dalili za Sunnah za kinabii zinazoonyesha kuwa ni lazima kwa mwanamke kufunika uso wake mbele ya wasiokuwa Mahram zake ni ile Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia:

“Wapanda farasi wanaume walikuwa wakitupitia na sisi tuko kwenye Ihraam pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanapotujongelea, kila mmoja wetu anateremsha mavazi yake ya juu, Jilbaab, usoni mwake. Wanapokuwa wameshapita, tunajifunua tena.”

Ameipokea Ahmad, Abu Daawuud na Ibn Maajah.

Dalili za uwajibu wa mwanamke kufunika uso wake mbele ya wasiokuwa Mahram zake kutoka katika Qur-aan na Sunnah ni nyingi. Napendekeza kwako dada muislamu kusoma kitabu “al-Hijaab wal-Libaas fiys-Swalaah” cha Ibn Taymiyyah, kitabu “al-Hijaab” cha Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz, kitabu “as-Swaarim al-Mash-huur ´alaa al-Muftiyniyna bis-Sufuur” cha Shaykh Hamuud at-Tuwayjiriy na kitabu “al-Hijaab” cha Shaykh Swaalih bin ´Uthaymiyn. Vitabu hivi ndani yake mna yenye kutosheleza.

Ee dada wa Kiislamu! Tambua kwamba wale wanachuoni waliokujuzishia kuonyesha uso – pamoja na kwamba maoni yao ni dhaifu – lakini wameliwekea sharti ya kuaminika na fitina. Fitina si yenye kuaminika na khaswa katika zama hizi ambazo msukumo wa kidini kwa wanaume na wanawake umekuwa mdogo, haya imekuwa ndogo, walinganizi wa fitina wamekuwa wengi, wanawake wametafanuni kwa kuweka aina mbalimbali za mapambo kwenye nyuso zao, mambo ambayo yanaita katika fitina. Hivyo basi dada wa Kiislamu! Tahadhari kutokamana na hayo. Lazimiana na Hijaab itayokukinga kutokamana na fitina kwa idhini ya Allaah. Hakuna mwanachuoni yeyote wa Kiislamu, tokea hapo zamani hadi hii leo, ambaye anawajuzishia wanawake hawa waliofitiniwa yale waliyotumbukia ndani yake hii leo.

[1] 24:31

[2] 33:53

[3] 33:53

[4] 33:59

[5] (22/110-111).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 49-52
  • Imechapishwa: 31/10/2019