24. Uwajibu wa kutengeneza sehemu ya kuogea/tiba katika nyumba

22- Uwajibu wa kutengeneza sehemu ya kuogea/tiba nyumbani

Ni wajibu kwa mume na mke kutenga sehemu ya kuogea katika nyumba yao. Mume asimruhusu mke kwenda kuoga katika vyoo vya nje. Jambo hilo ni haramu. Juu ya hilo kuna Hadiyth zifuatazo:

1- Jabiyr (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho, basi asimwache mkewe kuingia katika vyoo vya nje, yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho, basi asende bafuni isipokuwa awe na izari [nguo ya kiunoni], yule mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho, basi asiketi kwenye meza kunakohudumiwa pombe.”[1]

2- Umm Dardaa´ amesema:

“Nilitoka kwenda sehemu ya kuogea ambapo nikawa nimekutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema:

“Unaelekea wapi, ee Umm Dardaa´?” Nikajibu: “Sehemu ya kuogea.” Akasema: “Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake ya kwamba hakuna mwanamke yeyote ambaye anavua nguo – isipokuwa katika nyumba ya mmoja katika mama zake – ila amekiuka kila stara iliyoko kati yake na ar-Rahmaan.”[2]

3- Ibn Mulayh amesema:

“Kuna wanawake kutoka Shaam waliingia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambapo akawauliza: “Nyinyi ni wa wapi?” Wakajibu: “Kutoka Shaam.” Akasema: “Huenda nyinyi mnatoka katika vitongoji ambavyo vinawaruhusu wanawake wao kutoka katika vyoo vya nje?” Wakasema: “Ndio.” Akasema: “Hakika mimi nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Hakuna mwanamke yeyote ambaye anavua nguo nje ya nyumba yake isipokuwa amekiuka kila stara iliyoko kati yake na Allaah (Ta´ala).”[3]

[1] Ameipokea al-Haakim katika (04/288) na matamshi ni yake, at-Tirmidhiy na sehemu yake nyingine ni an-Nasaa´iy, Ahmad (03/339), al-Jurjaaniy (150) kupitia njia zengine. Abu az-Zubayr amepokea kutoka kwa Jaabir. al-Haakim amesema: “Ni Swahiyh juu ya masharti ya Muslim.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye na at-Tirmidhiy amesema: “Ni Hadiyth nzuri.” Ina shawahidi nyingi ambazo unaweza kuziona katika at-Targhiyb wat-Tarhiyb (01-89-91).

[2] Ameipokea Ahmad (06-361-362), ad-Dawlaabiy (02/134) kwa sanadi mbili ambapo moja wapo ni Swahiyh na al-Mundhiriy ameipa nguvu.

[3] Wameipokea waandishi wa “as-Sunan” isipokuwa an-Nasaa´iy, ad-Daarimiy, at-Twayaalisiy, Ahmad, Ibn A´raabiy katika “al-Mu´jamah” yake (01/71), al-Haakim (04/288) na wengineo.

Katika Hadiyth hii kuna Radd kwa wale wanaosema:

“Hakuna Hadiyth iliyosihi kuhusu kutoka katika vyoo vya nje.”

kama mfano wa Ibn-ul-Qayyim katika “Zaad” (01/62). Hakutumbukia katika hilo isipokuwa ni kwa sababu ya kutegemea baadhi ya njia za Hadiyth hii na kutofanya utafiti juu ya njia zake zengine.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 140-141
  • Imechapishwa: 19/03/2018