24. Tafsiri ya Hadiyth ya Asmaa´

2- Hadiyth ya ´Aaishah ni dhaifu kutokana na sababu mbili:

Ya kwanza: Kuna mkato baina ya ´Aaishah na Khaalid bin Jurayk ambaye amepokea kutoka kwake. Kasoro hiyo ameiashiria Abu Daawuud mwenyewe pale aliposema:

“Khaalid bin Jurayk hakusikia kitu kutoka kwa ´Aaishah.”

Abu Haatim ar-Raaziy amesema pia kuwa Hadiyth ina kasoro.

Ya pili: Kwenye mnyororo kuna Sa´iyd bin Bashiyr an-Naswriy ambaye alikuwa anaishi Damascus. Ibn Mahdiy na ukiongezea juu yake Ahmad wameacha mapokezi yake, Ibn Ma´iyn, Ibn-ul-Madiyniy na an-Nasaa´iy wamesema alikuwa ni dhaifu. Hivyo basi Hadiyth ni dhaifu na haiwezi kusimama na zile Hadiyth Swahiyh zinazowajibisha kujifunika.

Isitoshe jengine ni kwamba Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa na miaka ishirini na saba wakati wa Hijrah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa ni mwanamke mkubwa. Ni jambo lisilowezekana akaingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amevaa mavazi ya kubana yenye kuonesha zaidi ya uso na mikono na Allaah ndiye anajua zaidi. Na kama itakuwa Swahiyh basi ni lazima tukio hili liwe limetokea kabla ya kufaradhishwa Hijaab. Kwa sababu dalili za kujifunika ni zenye kutanua zaidi kutoka kwenye kianzio, kama tulivyotangulia kusema.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 26/03/2017