1 – Ni lazima kwa vazi la mwanamke wa Kiislamu liwe pana linalomfunika mwili wake mzima mbele ya wanaume ambao sio Mahram zake. Asijifunue mbele ya Mahram zake mbali na yale ambayo kidesturi yamezoeleka kufunuliwa kama vile uso wake, viganja vyake vya mikono na miguu yake.

2 – Liwe ni lenye kusitiri yaliyo nyuma yake. Lisiwe ni jepesi kiasi cha kwamba linaonyesha nyuma yake rangi ya ngozi yake.

3 – Lisiwe ni lenye kubana kwa njia ya kwamba linaonyesha fomu ya viungo vyake. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna watu aina mbili wa Motoni sijawaona; wanawake waliovaa vibaya, uchi, Maaylaat na Mumiylaat. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Hawatoingia Peponi na wala hawatonusa harufu yake na wanaume walio na bakora kama mkia wa ng´ombe ambazo wanawapiga kwazo waja wa Allaah.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “waliovaa vibaya, uchi” yamefasiriwa kwamba anavaa yasiyomsitiri. Amevaa lakini ukweli wa mambo ni kwamba yuko uchi. Ni kama mfano wa ambaye amavaa nguo nyembamba ambayo inaonyesha ngozi yake au nguo yenye kubana ambayo inaonyesha fomu ya viungo vyake kama mfano wa kiuno chake, mkono wake na mfano wake. Vazi la mwanamke ni lile linalomsitiri ambalo halionyeshi mwili wake wala fomu ya viungo vyake kwa sababu ni nene na pana.”[1]

4 – Asijifananishe na wanaume katika mavazi yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke anayejifananisha na wanaume na mwanamke anayejifanya dume. Mwanamke kujifananisha na wanaume ni kwa kule yeye kuvaa mavazi ambayo kiaina na namna ni maalum kwa wanaume pekee kutegemea na desturi za kila jamii. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Tofauti kati ya mavazi ya wanaume na mavazi ya wanawake ni jambo linarejea juu ya yale yanayosilihi kwa wanaume na yale yanayosilihi kwa wanawake. Ni yale yanayonasibiana na yale aliyoamrishwa mwanaume na yale aliyoamrishwa mwanamke; wanawake wameamrishwa kujisitiri na kuvaa Hijaab pasi na kuonyesha mapambo na kujionyesha. Kwa ajili hii ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah kwa mwanamke kunyanyua sauti yake katika adhaana, kuleta Talbiyah, wala kupanda juu ya mlima Swafaa na Marwah, wala kujiepusha na mavazi mengine kwenye Ihraam kama anavyojiepusha mwanaume. Mwanaume ameamrishwa kufunua kichwa chake na wala asivae mavazi yaliyozoeleka; nayo ni zile zilizotengenezwa kwa kiasi cha viungo vyake. Kwa hivyo hatakiwi kuvaa kanzu, suruwali, kofia za kanzu wala viatu.” Mpaka aliposema: “Kuhusu mwanamke hakukatazwa chochote katika mavazi. Kwa sababu ameamrishwa kujisitiri na kuvaa Hijaab. Kinyume na hayo hayakuwekwa katika Shari´ah. Lakini amekatazwa kuvaa Niqaab na vifuniko vya mikono. Kwa sababu hayo ni mavazi yaliyotengenezwa kwa kiasi cha viungo na wala hayahitajii.” Kisha akataja kwamba anatakiwa kufunika uso wake kwa kitu kingine mbele ya wanaume. Mpaka akasema mwishoni: “Kukishabaini kwamba ni lazima kuwe na tofauti kati ya mavazi ya wanaume na mavazi ya wanawake ambayo wanaume watapambanuka kutokamana na wanawake na mavazi ya wanawake yawe na sitara na kujifunika ambayo yanapatikana makusudio ya hayo, hapo yatadhihiri malengo ya mlango huu. Jengine ni kwamba kumebainika kwamba mavazi ikiwa mara nyingi ni kuvaliwa na wanaume basi wanawake watakatazwa nayo.” Mpaka aliposema: “Ikiwa mavazi yamekusanya uchache wa kujisitiri na kujifananisha, basi litakatazwa kwa njia zote mbili. Allaah ndiye anajua zaidi.”[2]

5 – Lisiwe na mapambo yanayozungusha macho ya wanaume wakati anapotoka nyumbani ili asiwe miongoni mwa wale wenye kuonyesha mapambo.

[1] (22/146).

[2] (22/148-155).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 45-49
  • Imechapishwa: 31/10/2019