24. Njiia ya Salaf imekusanya kheri zote


100- Khabari sahihi zinazothibitisha sifa za Allaah (Ta´ala) ni Swahiyh na zilizothibiti kwa nukuu za watu waadilifu na waaminifu waliokubaliwa na Salaf. Salaf walizinakili na hawakuzipinga wala kuzitia dosari.

Kuhusu Hadiyth zilizotungwa (ambazo zilitungwa na mazanadiki ili kuwababaisha waislamu) au Hadiyth dhaifu, haijuzu kuziamini wala kuziitakidi. Bali uwepo wake ni kama kutokuwepo kwake. Yale yaliyozuliwa na mazanadiki ni kama itikadi wanayojinasibisha nayo.

101- Wale watambuzi wanapaswa kufuata zile sahihi na kuchana na nyenginezo. Mtu wa kawaida atalazimika kuwaigiliza na kuwauliza wanachuoni, kwani Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Hivyo basi waulizeni watu wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.”[1]

Akitatizwa na kitu na asipate wa kumuuliza, basi anatakiwa kuchukua msimamo wa kukomeka na aseme kuwa anaamini yale yaliyosemwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pasi na kuthibitisha kitu. Kama hayo yanayonasibishwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yamesemwa naye, basi ameyaamini na kama hayakusemwa naye basi hakuyaamini. Haya yanakumbushia maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yale wanayokuelezeni watu wa Kitabu basi msiwasadikishe na wala msiwakadhibishe. Badala yake semeni: “Tumeamini yale tuliyoteremshwa kwetu na yakateremshwa kwenu.”[2]

102- Akawakataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusadikisha kwa kuchelea isije kuwa wongo. Na akawakataza kukadhibisha kwa kuchelea isije kuwa kweli. Badala yake akawaamrisha kusema yale yanayopelekea kuamini yale yaliyo ya haki peke yake. Hayohayo ndio yanayoweza kusemwa juu ya maudhui haya.

103- Aidha Hadiyth hizi hapana haja ya kutendewa kazi wala hukumu inayosomwa kutoka humo. Inatosha kwa mtu kuamini yale yaliyomo ndani yake.

104- Jengine litambulike ni kwamba ambaye anathibitisha sifa kutoka katika Hadiyth hizi zilizotungwa ni mbaya zaidi kuliko yule ambaye amepindisha maana ya Hadiyth Swahiyh. Dini ya Allaah (Ta´ala) iko kati ya yule mwenye kuchupa mpaka na mwenye kuzembea na njia ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) imekusanya kheri zote. Allaah atuwafikishe sisi na nyinyi kuifuata. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] 16:43

[2] Ahmad (4/136), Abu Daawuud (3644) na Ibn Hibbaan (110).

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta'wiyl, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 14/01/2021