24. Ni ipi hukumu ya kujinasibisha na baadhi ya makundi yaliyotujia, kuyasapoti na kuyatetea?

Swali 24: Ni ipi hukumu ya kujinasibisha na baadhi ya makundi yaliyotujia, kuyanusuru na kuyatetea?

Jibu: Nchi hii ina kundi moja tu. Limejengwa juu ya Tawhiyd na Uislamu na liko chini ya uongozi wa Kiislamu. Nchi ina amani na utulivu na kuna kheri nyingi. Sisi ni kundi moja tu na wala hatukubali migawanyiko. Uwepo wa makundi mengi ni jambo linapatikana katika nchi nyinginezo ambazo hamna utulivu wa kisawa na usalama. Kuhusu nchi yetu inatofautiana na nchi nyinginezo kwa sababu Allaah ameitunukia ulinganizi wa Tawhiyd, kutokuwepo shirki na serikali ya Kiislamu inayohukumu kwa Shari´ah. Hali ilikuwa namna hiyo tokea wakati wa Imaam na muhuishaji Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) mpaka hii leo – na himdi zote njema anastahiki Allaah.

Hatusemi kuwa nchi imekamilika katika pande zote, lakini pamoja na hivyo bado imesimama juu ya kheri. Kunaamrishwa mema na kukatazwa maovu. Kunasimamishwa adhabu za Kishari´ah. Hukumu ni kwa mujibu wa yale aliyoteremsha Allaah. Mirathi inagawanywa kwa mujibu wa Shari´ah ya Allaah. Hakuna yeyote ana haki ya kuliingilia hilo. Tofauti na nchi nyengienezo.

Sisi ni kundi moja tu katika nchi hii. Hatukubali makundi na madhehebu mengine yenye kwenda kinyume na madhehebu ya Salaf. Kwa sababu yanatufarikisha sisi sote, yanatia sumu kwenye fikira za vijana na kusababisha uadui na chuki kati yetu[1]. Makundi haya yakituingilia, basi tutakosa neema hii ambayo hivi sasa tunaishi ndani yake[2]. Hatuyataki makundi haya. Kheri inayopatikana katika makundi hayo sisi tuko nayo na zaidi. Shari inayopatikana humo sisi hatuitaki. Ni wajibu[3] kwetu kuwapa watu kheri.

[1] Baadhi ya fikira za vijana zimetiwa sumu kwa sababu ya  mapote haya ya kizushi, madhehebu ya kuangamiza na Hizbiyyah inayochukiza. Matokeo yake chuki ikawa ya wazi kati ya vijana wengi. Hali imefikia kiasi cha kwamba ndugu wa damu wamefikia kuchukiana katika nyumba moja. Mmoja anajinasibisha na pote fulani analopenda na kuchukia kwa ajili yake, mwengine anajinasibisha na pote lingine analopenda na kuchukia kwa ajili yake. Sivyo tu, bali hata walinganizi wameanza kuchukiana kwa sababu kujinasibishaji na Hizbiyyah na matamanio potofu. Allaah amrehemu Shaykh-ul-Islaam ambaye amesema.

“Bid´ah zimefungamanishwa na mfarakano na Sunnah imefungamanishwa na mkusanyiko. Ndio maana kunasemwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Ahl-ul-Bid´ah wal-Furqah.” (al-Istiqaamah (01/41))

[2] Mapote ya kivyamavyama ya kisasa kama vile Jamaa´at-ut-Tabliygh, al-Ikhwaan al-Muslimuun, Qutbiyyah, Suruuriyyah na Haddaadiyyah ni miongoni mwa mapote yaliyotuingilia. Walinganizi wa Salafiyyah ambao wanajinasibisha na mfumo wa Salaf na kufuata mapokezi ni wajibu kwao kupambana na mapote haya ya kizushi yanayoenda kinyume na yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Haitakikani kuwapa nafasi mifumo yao ikatanua, bali ni wajibu kuwabana na kukata mizizi zao kwa kueneza elimu ya Kishari´ah kwa mujibu wa dalili ya Qur-aan na Sunnah na juu ya ufahamu wa Salaf. Watu wanatakiwa kufunzwa Tawhiyd ambayo mapote haya wanaipuuza na kuwashughulisha watu n siasa na hamasa za kisiasa.

Baadhi ya watu wametilia umuhimu, kama wanavyodai wenyewe, kuwaokoa watu na maasi na kuwaingiza misikitini na wakati huohuo wanawaacha wabaki na I´tiqaad zao za kishirki pale wanapowaacha kuyapapasa makaburi kwa ajili ya kutafuta baraka, kuyazunguka na kuwataka uokozi wenye nayo.

Wengine wametilia umuhimu, kama wanavyodai wenyewe, kuleta umoja na kusameheana katika mambo ya tofauti za ´Aqiydah. Kwa sababu wanaonelea kuwa ´Aqiydah inafarikisha ummah. Ndio maana utawaona waabudia makaburi, Khawaarij, Mu´tazilah, Jahmiyyah na Shiy´ah wako kati yao. Mfumo wao unahusiana na kukusanya tu. Wanachotilia umuhimu tu ni kutaka kukusanya idadi kubwa ya wafuasi. Kanuni yao ni:

“Tushirikiane sote kwa pamoja katika yale tunayokubaliana na kupeana udhuru katika yale tunayotofautiana.”

Ni lazima kwa Ahl-us-Sunnah wal-Athar, Salafiyyuun, kuzifichua hali za mapote haya yenye kwenda kinyume, kuutahadharisha ummah kutokana nayo, kuraddi hoja zao tata na kuyaponda kwa dalili za Kishari´ah. Kadhalika ni juu yao kulingania katika mfumo wa Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) na kupandikiza ´Aqiydah ya Salafiyyah kwenye mioyo ya vizazi vinavyokuja huko mbele kama ambavyo wahenga wetu waliipanda ndani ya mioyo yetu.

[3] Huku ni kwa njia ya kuelezea neema ya Allaah juu yetu katika Tawhiyd, wanazuoni wenye kushikamana na Salaf na watawala wenye kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah na waliofanya marejeo ni kurudi katika Qur-aan na Sunnah na sio sheria zilizotungwa na wanaadamu – na himdi zote njema zinamstahikia Allaah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 66-68
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy