24. Makatazo ya kusimama katika suala la Qur-aan

Imaam Ahmad amesema:

“Mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa au akasimama na kusema:

“Mimi sijui kama matamshi yameumbwa au hayakuumbwa – Qur-aan ni maneno ya Allaah tu.”

ni mtu wa Bid´ah sawa na yule mwenye kusema kuwa imeumbwa. Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa.”

Wakati ilipokuja fitina ya kuumbwa kwa Qur-aan na kukatokea mtengano kati ya Ahl-us-Sunnah na Jahmiyyah, Mu´tazilah na wengine, ndipo kulijitokeza watu wenye kujinasibisha na Ahl-us-Sunnah wenye kusema:

“Qur-aan ni maneno ya Allaah, lakini matamshi yangu yameumbwa.”

Imaam Ahmad akawakemea kwa sababu neno “matamshi” kunaweza kukusudiwa kile kinachotamkwa, ambayo ni Qur-aan, kama ambavyo kunaweza kukusudiwa pia matamshi ya msomaji. Maneno haya yanaweza kufahamika vibaya na Jahmiyyah, Mu´tazilah na wengine wenye kusema kuwa Qur-aan imeumbwa wanaweza kuyatumia kama fursa ili kuwapoteza watu. Ndio maana Ahmad akamfanyia Tabdiy´ anayesema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa.

Unasema kuwa maneno ya Allaah hayakuumbwa. Usisemi kuwa matamshi yako ya Qur-aan yameumbwa. Watu wa batili wanaweza kuyatumia ili waweze kufikia kuwa Qur-aan imeumbwa. Wala usisimame; kuwa ni mwenye maazimio. Azimia ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa, kama inavyoafikiana na Qur-aan, Sunnah, Maswahabah na Salaf-us-Swaalih. Mwenye kusimama anashakiwa Bid´ah na kuwa na madhehebu ya Jahmiyyah. Maneno haya, Bid´ah hizi na mambo ya kusimama yalizuka wakati kulipotokea fitina hii na kukua. Ni lazima kusema kuweka wazi na kusema kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa. Usisemi kuwa matamshi yako ya Qur-aan yameumbwa na wala usisimame. Haijuzu kusimama na wala haijuzu kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa.

Watu wengi walisema kuwa hawajui kama Qur-aan imeumbwa au haikuumbwa. Ahmad na Ahl-us-Sunnah wakawaangusha na kuwafanyia Tabdiy´ kwa ajili ya hilo. Mmoja wao alikuwa ni Ya´quub bin Shaybah ambaye alikuwa ni Imaam katika Hadiyth. Aliposimama katika suala la Qur-aan na kusema kuwa hajui kuwa imeumbwa au haikuumbwa Ahmad akasema:

“Ni mtu wa Bid´ah mpotevu.”

Wakati khaliyfah alipomtaka ushauri Ahmad juu ya kumpa cheo Ya´quub bin Shaybah mahakamani akasema:

“Hapana. Ni mpotevu.”

Huenda mkastaajabu na hili. Ahmad anampa kipaumbele myahudi na mnaswara kufanya kazi kabla ya Ahl-ul-Bid´ah kutokana na khatari zao.  Ahl-ul-Bid´ah wanaibomoa na kuiharibu jamii kwa ndani. Ni kina nani wengine waliowaharibu waislamu na kusababisha wakaanguka mbele ya mayahudi na manaswara kama sio Ahl-ul-Bid´ah? Majanga yote yaliyowafika waislamu ni kwa sababu ya Ahl-ul-Bid´ah. Dola ya Banuu Umayyah ilianguka wakati khaliyfah wake Marwaan al-Himaar alipotumbukia katika madhehebu ya al-Ja´d, yamesemwa na Ibn Taymiyyah. Bid´ah hii si lolote ukilinganisha na Bid´ah zingine zote zilizoko hii leo.

Imaam Ahmad amesema:

“… ni mtu wa Bid´ah sawa na yule mwenye kusema kuwa imeumbwa. Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa.”

Bi maana yule mwenye kusimama na mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa. Ni katika mkumbo mmoja.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 386-387
  • Imechapishwa: 13/08/2017